Mbowe Aomba Maridhiano na JPM – Video


MWENYEKITI wa Chama cha Demokrasia Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe amesema sababu za kushiriki katika sherehe za maadhimisho ya miaka 58 ya uhuru wa Tanganyika (Tanzania Bara) ni kutoa ujumbe wa kuwepo kwa ulazima wa maridhiano, upendo na mshikamano.



Ametoa ujumbe huo leo Desemba 9, 2019 katika sherehe hizo zilizofanyika kitaifa katika Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza baada ya kupewa nafasi na Rais Magufuli kutoa salamu zake kama kiongozi wa chama cha siasa, akiongozana na wanasiasa wengine waliohudhuria sherehe hizo.



“Nimekuja kushiriki sherehe za miaka 58 ya Uhuru kama uthibitisho wa ulazima wa kuwepo maridhiano, upendo, mshikamano katika taifa letu. Namuomba Mungu siku ya leo ikafungue milango tuweze kuishi kama taifa linalopendana, tuvumiliane, tukosoane, turuhusu demokrasia.

”Rais una nafasi ya kipekee kuweka historia ya maridhiano katika taifa letu kwani kuna wengine wanalalamika wanaumia. Rais tumia nafasi hii ukaliweke taifa katika hali ya utengamano,” amesema Mbowe.

Mbowe ameshiriki katika maadhimisho hayo huku akiwa na kesi ya uchochezi mahakamani kwa zaidi ya miaka sasa, sambamba viongozi wenzake nane, lakini pia kukiwa na zuio la kutofanya mikatano ya hadhara.

Pia, kumekuwa na malalamiko ya vyama vya upinzani kuhusu kubinywa kwa demokrasia nchini, hivyo ujumbe wa Mbowe unamuomba Rais Magufuli kujenga maridhiano kati ya serikali ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) na wapinzani.

Mbali na Mbowe, viongozi wengine wa Chadema waliohudhuria sherehe hizo ni Mwenyekiti wa chama hicho Kanda ya Kati, Lazaro Nyalandu; Naibu Katibu Mkuu wa Chadema Bara na Mbunge wa Kibamba, John Mnyik;  na Mwenyekiti wa Chadema Kanda ya Kaskazini, Godbless Lema; Mbunge wa Tarime Vijijini, John Heche na wengine.


Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad