Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe amempongeza Rais John Magufuli kutokana na juhudi mbalimbali anazozifanya katika kuliongoza taifa.
Akizungumza katika maadhimisho ya sherehe za miaka 58 ya uhuru wa Tanzania bara yaliyofanyika kitaifa jijini Mwanza, katika Uwanja wa CCM Kirumba, Mbowe amesema kuna ulazima wa kuwepo maridhiano na mshikamano ili taifa lizidi kusonga mbele.
“Nimekuja kushiriki sherehe za miaka 58 ya uhuru kama udhibitisho wa ulazima wa kuwepo maridhiano, upendo na mshikamano katika taifa letu, ninamuomba Mwenyezi Mungu siku ya leo ikafungue milango tuweze kuishi kama taifa linalopendana, tuvumiliane, tukosoane, turuhusu demokrasia ili tujenge taifa lenye upendo na mshikamano.
“Mheshimiwa rais una nafasi ya kipekee kuweka historia ya maridhiano katika taifa kwani kuna wengine wanalalamika na kuumia basi utumie nafasi hii kuliweka taifa katika nafasi ya utengamano,” amesema Mbowe.
Mbali na Mbowe, viongozi wengine waliopata nafasi ya kuzungumza na maelfu ya wananchi waliojitokeza katika uwanja huo ni Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF) Profesa Ibrahim Lipumba ambapo amesema kuna haja ya serikali kuimarisha demokrasia hasa wakati tukijiandaa kulekea katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2020.
"Ninampongeza Rais (Dkt Magufuli) kwa kazi aliyofanya, lakini ninamuomba ajue ana jumuku la kujenga demokrasia katika nchi yetu, hasa tunapoelekea uchaguzi wa mwaka 2020."Amesema Lipumba