Mbowe Mwenyekiti Tena CHADEMA, Lissu Makamu wake


Dar es Salaam. Freeman Mbowe,  amechaguliwa tena kuwa mwenyekiti wa Chadema baada ya kupata kura 886 sawa na asilimia 93.5 huku mshindani wake  Cecil Mwambe akipata kura 59 sawa  na asilimia 6.2.

Katika uchaguzi wa mwaka 2014, Mbowe alipata kura 789 sawa na asilimia 97.3.

Matokeo hayo yametangazwa leo Alhamisi Desemba 19, 2019 saa 11 alfajiri na msimamizi wa uchaguzi, Sylvester Masinde, akibainisha kuwa kura tatu ziliharibika.

Uchaguzi huo umefanyika katika ukumbi wa Mlimani City jijini Dar es Salaam.

Wakati matokeo hayo yakitangazwa Mwambe hakuwepo ukumbini licha ya kuitwa zaidi ya mara tatu.

Baada ya Masinde kumtangaza Mbowe kuwa mshindi, idadi kubwa ya wajumbe wa mkutano mkuu  walinyanyuka kwenye viti  na kumfuata mbunge huyo wa Hai kwa ajili ya kumpongeza.


Walimbeba na kuanza kuzunguka naye huku na huko wakiimba nyimbo za matumaini, "Mbowe tuvushe, mwamba tuvushe," na kisha  kumpeleka jukwaa kuu alikokuwa ameketi katibu mkuu wa chama hicho, Dk Vicent Mashinji na wasimamizi wa uchaguzi.

Ratiba za uchaguzi huo zilianza jana asubuhi na wagombea walianza kujinadi saa 5 usiku, matokeo kutangazwa leo alfajiri.

Masinde amemtangaza mwanasheria mkuu wa chama hicho, Tundu Lissu  kuwa makamu mwenyekiti (Bara)  baada ya kupata kura 930 sawa na asilimia 98.8 na kumshinda mbunge wa Viti Maalum, Sophia Mwakagenda aliyejitoa wakati akiomba kura.

"Kwa kuwa Mwakagenda alitangaza kujitoa wakati wa kuomba kura lakini  karatasi za kura zilishawekwa jina lake kuna watu walitegemea kumpa kura na alipata 11."
Tags

Post a Comment

1 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.
  1. Ndivyo tulivyotegema Mbowe ni mfalme sio mwenyekiti hiyo ndio demokrasia ya kuwa mwenye kiti Maisha yoye

    ReplyDelete

Top Post Ad

Below Post Ad