Mbwana Samatta Atemwa Tuzo za Afrika


Ukanda wa Afrika mashariki hautokua na mwakilishi yoyote kwenye kinyang’anyiro cha kuwania tuzo za wachezaji bora, zinazoandaliwa na shirikisho la soka barani Afrika CAF.

Hali hiyo imedhihirika baada ya mchujo kufanywa na kisha orodha ya majina ya wachezaji waliosalia kwenye kinyang’anyiro hicho kutolewa na shirikisho la soka barani Afrika, kuelekea kilele cha tuzo Januari 07, 2020.

Timu ya taifa ya wanawake ya Kenya (Harambee Starlets) imeondolewa kwenye orodha ya kipengele cha tuzo ya timu bora ya mwaka kwa wanawake.

Kenya ilikua nchi pekee katika ukanda wa Afrika mashariki iliyoingia kwenye kipengele hicho, huku timu za mataifa ya Zambia, Nigeria, Ivory Coast, Cameroon na Afrika kusini zikisalia.

 Kocha mkuu wa timu ya Harambee Starlets David Ouma pia ameondolewa kwenye orodha ya makocha wanaowania tuzo ya kocha bora wa mwaka 2019 na kuwaacha Alain Djeumfa wa Cameroon, Bruce Mwape wa Zambia, Clementine Toure wa Ivory Coast, Desiree Ellis wa Afrika Kusini pamoja na Thomas Dennerby wa Nigeria.

Katika hatua nyingine nahodha na mshambuliaji wa timu ya taifa ya Tanzania (Taifa Stars) Mbwana Samatta na mlinda mlango wa kikosi cha Uganda Denis Onyango, nao wametemwa kwenye orodha ya wachezaji wanaowania tuzo ya mchezaji bora wa Afrika.

Mshambuliaji wa klabu ya Simba na timu ya taifa ya Rwanda Meddie Kagere pamoja na Emmanuel Okwi wa Uganda, nao pia wameondolewa kwenye kinyang’anyiro cha kuwania tuzo ya mchezaji bora upande wa kalbu za Afrika.

 Orodha kamili ya wanaowania tuzo baada ya kufanyika mchujo.

Mchezaji bora wa Afrika: André Onana (Cameroon & Ajax), Hakim Ziyech (Morocco & Ajax), Ismail Bennacer (Algeria & AC Milan), Kalidou Koulibaly (Senegal & Napoli), Mohamed Salah (Egypt & Liverpool), Odion Ighalo (Nigeria & Shanghai Shenhua), Pierre-Emerick Aubameyang (Gabon & Arsenal), Riyad Mahrez (Algeria & Manchester City), Sadio Mane (Senegal & Liverpool) na Youcef Belaili (Algeria & Ahli Jeddah).

Mchezaji bora wa Afrika kwa wanawake: Ajara Nchout (Cameroon & Valerenga): Asisat Oshoala (Nigeria & Barcelona), Gabrielle Onguene (Cameroon & CSKA Moscow), Tabitha Chawinga (Malawi & Jiangsu Suning) na Thembi Kgatlana (South Africa & Beijing Phoenix FC).

Mchezaji bora wa Afrika (Interclubs Player of the Year): Anice Badri (Tunisia & Esperance), Kodjo Fo Doh Laba (Togo & RS Berkane / Al Ain), Taha Yassine Khenissi (Tunisia & Esperance), Tarek Hamed (Egypt & Zamalek)na Youcef Belaïli (Algeria & Esperance/Ahli Jeddah).

Mchezaji bora kijana wa Afrika: Achraf Hakimi (Morocco & Borussia Dortmund), Krépin Diatta (Senegal & Club Brugge), Moussa Djenepo (Mali & Southampton), Samuel Chukwueze (Nigeria & Villarreal), Victor Osimhen (Nigeria & Lille).

Kocha bora wa Afrika kwa wanaume: Aliou Cisse (Senegal – Senegal), Christian Gross (Switzerland – Zamalek), Djamel Belmadi (Algeria – Algeria), Moïne Chaâbani (Tunisia – Esperance) na Nicolas Dupuis (France – Madagascar).

Kocha bora wa Afrika kwa wanawake: Alain Djeumfa (Cameroon), Bruce Mwape (Zambia), Clementine Toure (Côte d’Ivoire), Desiree Ellis (South Africa) na Thomas Dennerby (Nigeria).

Timu bora ya taifa kwa Afrika kwa wanaume: Algeria, Madagascar, Nigeria, Senegal na Tunisia.

Timu bora ya taifa kwa Afrika kwa wanawake: Cameroon, Côte d’Ivoire, Nigeria, South Africa na Zambia.

Kilele cha kuwatangaza washindi kinatarajiwa kufanyika Januari 07, 2020 mjini Hurghada, Misri.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad