Mhadhiri mmoja wa chuo kikuu nchini Pakistan amehukumiwa kifo kwa kosa la kuikashifu dini ya kiislamu.
Junaid Hafeez mwenye umri wa miaka 33, alikamatwa mwezi Machi 2013 na kushutumiwa kutoa maoni yanayomkashifu mtume Muhammad katika mitandao ya kijamii.
Madai ya kudhihaki dini nchini Pakistan huwa yanachukuliwa na uzito wa juu na kufanya mtu aliyepewa shutuma hizo kuwa katika wakati mgumu.
Wakili wa kwanza wa bwana Hafeez , Bwana Rashid Rehman alipigwa risasi na kuuwawa mwaka 2014 baada ya kukubali kumtetea mtuhumiwa.
Mhadhiri huyo ambaye amekaa kizuizini kwa miaka kadhaa baada ya mashambulio yaliyofanywa na wafungwa wengine mara kadhaa.
Maamuzi ya mahakama yalitolewa katika mahakama ya Mutani iliyopo katikati ya mji, karibu na eneo ambalo bwana Hafeez alikuwa ameshikiliwa.
Bwana Hafeez alikuwa alisoma shahada yake ya pili nchini Marekani baada ya kupata ufadhili, baadae alibobea kwenye masomo ya lugha , picha na maonyesho ya majukwaani.
Baada ya kurejea Pakistan alianza kufundisha chuo kikuu cha Bahauddin Zakariya University (BZU) huko Multan, chuo ambacho alifanya kazi mpaka alipokamatwa.
Mawakili wakisheherekea uamuzi uliosomwa na mahakama
Msimamizi wa kesi ya Hafeez kwa sasa amesikitishwa na maamuzi hayo na kuliambia shirika la habari la AFP kuwa watakata rufaa dhidi ya maamuzi yaliyotolewa.
Wakati huohuo mawakili wa serikali walikuwa wanasheherekea maamuzi hayo ya hukumu ya kifo.
Shirika la kimataifa la Amnesty limesema uamuzi huo haukuwa wa haki na unasikitisha sana na kukatisha tamaa.
Sheria ya Pakistan inasema nini kuhusu mtu anayedhihaki dini?
Sheria ya Pakistan dhidi ya mtu anayedhihaki dini au kuitusi dini ya kiislamu, anastahili adhabu kali ikiwemo kifo.
Makosa yanayohusisha dini yalianzishwa na waingereza waliyoitawala India mwaka 1860 na kukua mwaka 1927. Pakistan ilirithi sheria hizi baada ya kutengana na India 1947.
Sheria hizi za awali ziliwekwa katika kipengele cha uhalifu ili kuhakikisha kuwa watu wanaheshimu dini, hawapiti kwenye makaburi, hawawatukani wanaoamini uwepo wa Mungu na kuheshimu maeneo ya kuabudu.
Chini ya sheria hizo, adhabu ilikuwa kati ya mwaka mmoja mpaka miaka 10 gerezani.
Lakini katikati ya mwaka 1980 na 1986, adhabu ziliongezwa na kamanda mkuu wa jeshi Zia-ul Haq.
Generali Haq alitaka sheria za waislamu na wasio waislamu zitenganizwe mwaka 1973, wakati idadi kubwa ya raia wa Pakistani ni waislamu.
Sheria hizo zilianzisha adhabu ya kifo au kifungo cha maisha kwa mtu yeyote anakaye mdhihaki mtume Muhammad.
Watu karibu 40 sasa wamehukumiwa hukumu ya kifo kwa kosa la kudhihaki dini ingawa hakuna aliyenyongwa mpaka sasa.
Mwaka jana mwezi Oktoba mahakama ya juu zaidi ya Pakistan ilibatilisha hukumu ya kifo kwa mwanamke mmoja wa kikristo aliyekutwa na hatia ya kuikashifu dini ya kiislamu.
Mahakama hiyo iliamuru kuachiwa huru kwa mwanamke huyo katika kesi ambayo iliigawa nchi.
Asia Bibi alifungwa mwaka 2010 baada ya kukutwa na hatia ya mashtaka kumkashifu mtume Muhammad baada ya kulumbana na majirani zake.
Mwanamke huyo alikuwa akisisitiza kuwa hana hatia lakini alitumikia kifungo cha miaka nane kwenye chumba cha peke yake jela.