KAIMU Kocha Mkuu wa Yanga, Boniface Mkwasa, amewapa masharti mazito nyota wapya wa Yanga waliotua kufanya majaribio kikosini hapo ambao wanatokea nchi za Eritrea, DR Congo na Malawi.
Yanga imepokea wachezaji wa kigeni wanne ambao ni viungo wawili, mshambuliaji mmoja na beki mmoja, huku Mkwasa akisisitiza kwamba mchezaji atakayepata nafasi kati ya hao, ni yule mwenye historia nzuri kisoka ikiwemo kucheza mechi nyingi za ligi alipotoka.
Kauli hiyo ya Mkwasa inamaanisha kwamba, wale wachezaji ambao tumezoea kuwaona kwenye YouTube wakionyesha makali yao lakini uwanjani hakuna kitu, hawatasajiliwa na Yanga katika kipindi hiki cha usajili wa dirisha dogo.
Yanga ipo katika mchakato wa kuboresha kikosi chao baada ya mapungufu yaliyojitokeza katika dirisha kubwa kwa baadhi ya nyota waliosajiliwa kutoka nje kutokuwa na faida kutokana na kutoitumikia vyema timu hiyo.
Taarifa ambazo Championi Ijumaa imezipata kutoka Yanga zinasema kuwa, Mkwasa ameonyesha msimamo wake katika dirisha dogo la usajili linalofunguliwa Desemba 16 kwa kuhakikisha nyota atakayepata saini ndani ya timu hiyo ni yule ambaye atakuwa amecheza mechi nyingi za ligi kwao na timu ya taifa na tofauti na hapo hakuna atakayepata nafasi.
“Kuna wachezaji wanne wametua kutoka Eritrea, DR Congo na Nigeria katika nafasi za ushambuliaji moja, viungo 2 na beki mmoja kwa ajili ya majaribio ambao watafanya kwa muda wa siku tatu ili kumpa nafasi mwalimu kumsajili atakayeona anafaa.
“Lakini Kocha Mkwasa amesisitiza kuwa mchezaji atakayepewa nafasi ya kusajiliwa Yanga ni yule ambaye atakuwa amecheza mechi nyingi kwenye ligi ya kwao na mechi za kimataifa,” alisema mtoa taarifa huyo.
Aidha, Championi Ijumaa lilimtafuta Mkwasa kuhusu suala hilo ambapo alisema kuwa kwa sasa hana nafasi ya kuzungumzia jambo hilo hadi wakati wake utakapofia.
Khadija Mngwai, Dar es Salaam