Msimuhukumu Maalim Seif kwa kuwa anapotoshwa na wanaomshauri - Katibu Mkuu CCM


Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi CCM Dkt. Bashiru Ally amesema, Maalimu Seif aliyekuwa kada wa CUF kabla ya kuhamia ACT, atumie elimu yake vizuri ajenge Chama Chake ili kiweze kushindana na CCM.

Ameyasema hayo wakati akizungumza na wanaCCM Mkoa wa Kusini Pemba alipokuwa akizundua tawi la Ole jimbo la Ole mara baada ya kufungua tawi hilo.

Amesema katika ziara yake ya siku tisa visiwa vya Unguja na Pemba, ina lengo la kuimarisha uhai wa Chama (kufunga mitambo) ya ushindi kwa uchaguzi wa mwaka 2020 hivyo, amesikitishwa na kauli ya Maalim Seif ya kukejeli ziara hiyo ambayo ipo kihalali na madhumini yake ni bayana.

“Maalim Seif hakuwahi kwenye matamko yake ama mikutano yake kunizungumzia kwa ukali na chuki kiasi kile kama alivyofanya, hivyo kama mitambo tu nimeifunga siku tisa mitetemeko hii imeanza kusababisha taharuki je ikianza kufanya kazi itakuaje? " alisema.

"Mimi sitaki kumjibu maana kwa bahati mbaya anawashauri wabaya kwa sababu kwa kasi ya ziara yake asingewezea kufuatilia bila kuwatuma watu, na ziara yangu kote imekuwa hadharani na vyombo vya habari vimekuwa vikiripoti, nimeshangaa kusikia mambo ambayo hayakutokea kwenye ziara yangu” Katibu Mkuu amesisitiza.

“Katika hili niwaase wanaCCM na watanzania msimuhukumu Maalim Seif kwa kuwa hata yeye anapotoshwa na wanaomshauri, tangu awe mshauri amekuwa hatafuti tena taarifa za kweli, kila anachopokea anakwenda kuropoka”. Ameongeza

Aidha, ametumia fursa hiyo kumuomba, ajenge chama chake kipya maana chama kile kinahitaji muda wa kutosha akianza kufukuzana na mitambo yake asilaumu kwenye masanduku ya kura atakapofungua na kukuta sifuri.

“Mimi ninatumia fursa hii kumshauri, Muda hauna huruma, muda hausubiri, kupoteza muda kufukuzana na mitambo ninayoifunga itamgharimu yeye na chama chake, hivyo awe na nidhamu ya muda na ajenge chama chake kichanga na Sisi tujenge chama chetu tukutane uwanjani.” Ameongeza

Dkt. Bashiru ameendelea kwa kueleza kuwa, watanzania wa leo na Tanzania ya Dkt. John Pombe Magufuli na Dkt. Ali Mohamed Shein hawadanganyiki tena wana macho yao na wanaona, na hasa vijana waliodanganywa kwa muda mrefu na wametumia hila nyingi sana kuwadanganya leo wametambua ukweli.
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad