Madrid, Hispania. Mwanamke mmoja nchini Hispania amezinduka baada ya moyo wake kusimama kwa sita.
Audrey Schoeman, anadaiwa moyo wake uliacha kufanyakazi kwa saa sita hivyo ndugu zake kudhani amefariki dunia.
Audrey alipata mshtuko wa moyo wakati anapanda mlima Pyrenees akiwa na mumewe mwezi Novemba.
Madaktari wanasema tukio la mwanamke huyo ndiyo la muda mrefu zaidi kwa moyo kusimama nchini Hispania.
Hata hivyo, mwanamke huyo ambaye anaendelea kupatiwa matababu alisema anatarajia kupanda tena mlima huo katika kipindi cha msimu wa masika.
Audrey mwenye umri wa miaka 34 anayeishi jijini Barcelona alianza kupata matatizo ya kuzungumza mara tu baada ya hali ya hewa kubadilika ghafla.
Kwa mujibu wa shirika la utangazaji la BBC, kadri alivyokuwa akipanda mlima aliishiwa nguvu na baadaye kupoteza fahamu.
“Niliamini amekufa baada ya hali yake kuzorota zaidi wakati akisubiri kupata huduma ya dharura,” alisema mume wa mwanamke huyo aliyetambulika kwa jina la Rohan Schoeman.
Akizungumza na vyombo vya habari Alhamisi iliyopita mwanaume huyo alisema “nilijaribu kugusa mapigo yake ya moyo hayakuwa yanapiga kabisa. Sikuweza kuhisi akipumua.”
Mwanaume huyo alisema saa mbili baadaye timu ya uokoaji ilifika eneo la tukio na kukuta joto lake la mwili likiwa limeshuka hadi nyuzi 18.
“Tulipowasili katika hospitali ya Vall d’Hebron, Barcelona hakukuwa na dalili zozote za kurejesha uhai wake, niliumia sana,” alisema.
Daktari Eduard Argudo aliyekuwa akimtibu Audrey alisema kiwango cha chini cha joto ambacho kilisababisha Audrey apoteze fahamu ndicho kilichonusuru maisha yake.
“Alionekana amekufa lakini tulikuwa na matumani atafufuka na kweli ikawa hivyo kwa sababu joto lililinda mwili na ubongo wake usizorote zaidi wakati akiwa amepoteza fahamu,” alisisitiza.
Alisema mwanamke huyo ataendelea kubaki hospitalini hapo mpaka pale atakapopata fahamu kabisa.