No title



MWANZA: Baba aliyejulikana kwa jina la Emmanuel Machumu (43), mkazi wa Mtaa wa Jiwe-Kuu, Kitangiri wilayani Ilemela jijini Mwanza, anadaiwa kuuawa na Polisi kufuatia kuhatarisha usalama wa watu, Gazeti la IJUMAA WIKIENDA lina mkasa mzima.

 

Machumu anadaiwa kuuawa na Polisi wiki iliyopita, ikiwa ni siku chache tangu alipotoka jela kwa msamaha wa Rais Dk John Pombe Magufuli ‘JPM’ wa Desemba 9, mwaka huu (Siku ya Uhuru).

 

MABISHANO NA POLISI

Kwa mujibu wa mashuhuda wa tukio hilo, Machumu alikutwa na umauti baada ya kutokea kwa mabishano ya muda mrefu kati yake na Polisi huku akitaka kuwateketeza watu kwa sime.

Mashuhuda hao walisema, Machumu alijikuta akishambuliana na Polisi baada ya kujeruhi watu kadhaa huku akimsaka Mtangazaji wa Kipindi cha Nitetee, Flora Lauwo kwa lengo la kumtoa uhai kwa sime.

 

FLORA ASIMULIA

Akilisimulia Gazeti la IJUMAA WIKIENDA mkasa mzima, Flora ambaye alinusurika kuuawa alisema kuwa, baba huyo alikuwa ametoka gerezani kwa msamaha wa Rais Magufuli akiwa ameshatumikia kifungo cha mwaka mmoja.

Alisema kuwa, Machumu alihukumiwa kwenda jela mwaka juzi, baada ya kukutwa na hatia ya unyanyasaji wa mtoto wake wa kumzaa wa kiume na pia jaribio la kumtoa kafara.

 

ANOA SIME SIKU TATU

Alisema kuwa, baada ya kutoka jela kwa msamaha hivi karibuni ndipo akaanza kunoa sime ambayo alianza kuitumia kujeruhi majirani na Polisi akimsaka Flora ili amuue.

“Huyu baba, baada ya kupata msamaha, alikuwa akisema kuwa lazima alipize kisasi kwa waliomfanya akaenda gerezani.

“Hivyo alipotoka tu jela, akaanza kunoa sime yake kwa siku tatu.

“Siku ya tukio, Maganga aliibeba sime hiyo, akawa anazunguka nayo mitaani.

 

ATAKA WATU

“Kuna jirani yake mmoja alimuuliza tu, unakwenda wapi na sime? Hapohapo akamkata nayo begani.

“Wakati anamshambulia jirani yake ndipo akajitokeza mwanaume mmoja ili kuamulia, lakini kilichompata hawezi kukisahau maisha yake yote yaliyosalia hapa duniani.

 

HALI MBAYA

“Yule aliyekwenda kuamulia aliishia kukatwa sime kichwani, tumboni na mkononi.

“Tunapozungumza hapa, huyo mtu ana hali mbaya mno hospitalini,” alisema Flora.

 

POLISI WAITWA

Flora aliendelea kusimulia kuwa, baada ya mashuhuda kuona vile, waliita Polisi ambao walifika mara moja na kuanza kutuliza vurugu.

Hata hivyo, Flora alisema kuwa, Polisi walimbembeleza mno Machumu asalimishe silaha hiyo, lakini aligoma na kuanza kuwakimbiza Polisi kwa sime.

 

MABOMU YA MACHOZI

Alisema kuwa, Polisi walipoona jamaa huyo anataka kuwakata, waliamua kurusha mabomu ya machozi, lakini bado aliendelea kuwakimbiza akitaka kuwakatakata.

“Yaani aligeuka kama mnyama kabisa. Kila Polisi walipojaribu kumsihi aweke silaha chini, alikataa na kusema lazima akalipize kisasi kwangu kwa kumchukua mwanaye na kingine kumfanya akateseke jela.

 

POLISI WALAZIMIKA KUMPIGA RISASI

“Polisi walipoona angeweza kuleta madhara makubwa kwa watu wengine ndipo wakalazimika kumpiga risasi na kufa hapohapo,” alisimulia Flora.

Flora alisema, majirani wa Machumu walimwambia kuwa alikuwa akisema akifika nyumbani kwake (kwa Flora) angemtenganisha kichwa na kiwiliwili na hapo angekuwa ametimiza haja yake ya kulipiza kisasi hicho.

 

“Lakini kabla hajafanya tukio hilo, yeye ndiye aliyepatwa na umauti huo.

 

“Mungu ana makusudi na mimi kwa kila jambo, kwa sababu hata nilivyomchukua mtoto huyo ni kwa sababu alikuwa akitaka kumtoa kafara na alikuwa anasali siku saba, ya nane ndiyo angemtoa kafara ndiyo majirani wakanipa habari, tukaenda pale na Polisi, wakamkamata na kuwekwa ndani kisha kuhukumiwa kwenda jela.

 

“Lakini sasa baada ya kupata msamaha wa JPM ndipo akaanza vurugu zake akitaka kulipiza kisasi na matokeo yake ameuawa,” alisema Flora.

 

KAMANDA MULIRO ATHIBITISHA

Akizungumza na Gazeti la IJUMAA WIKIENDA, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, ACP Muliro Jumanne alithibitisha kutokea kwa tukio hilo.

“Ni kweli tukio hilo limetokea na huyo mtuhumiwa alifariki dunia wakati anakimbizwa hospitalini,” alisema Kamanda Muliro.

 

HUKO NYUMA

Machumu aliwahi kuripotiwa na gazeti mama la hili, Uwazi baada ya kujitengenezea kaburi na kuliandika maneno mengi ya Biblia na kusema amejitayarishia makao mapema ili atakapokufa watu wasipate shida ya kutafuta sehemu ya kuzikwa.

Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad