Mwili bosi wa Zam Zam kuzikwa Dodoma, utata wagubika kifo chake



Dodoma. Mwili wa aliyekuwa mkurugenzi wa Shule za Zam Zam jijini Dodoma nchini Tanzania, Rashid Bura unatarajia kuzikwa leo mchana Alhamisi Desemba 26, 2019 katika makaburi ya Chamwino Dodoma.

Bura (60) alikutwa amekufa jana Jumatano Desemba 25, 2019 ofisini kwake eneo la Majani ya chai karibu na Nyerere square jijini humo huku mazingira ya kifo chake kikizua utata.

Rafiki wa karibu na mwanzilishi mwenzake wa Taasisi ya Dalai Islamiki Center, Abdillah Mboryo amesema mwili wa Bura umeharibika ni lazima wafanye haraka kumzika.

Mboryo amesema kwa mara ya mwisho Bura alionekana Jumapili jioni ya Desemba 22,2019 aliposali msikiti wa Nunge na baadaye aliwanunulia kahawa baadhi ya watu eneo la karibu.

Amesema jioni marehemu alimpigia simu Sheikh wa Mkoa wa Dodoma, Mustafa Rajab kumpa mrejesho wa kile kilichojiri katika mkutano wa amani uliofanyika jijini Dar es Salaam.

"Lakini baada ya hapo hakuonekana wala simu yake haikupatikana hadi jana mwili ulipokutwa ofisini ukiwa na majeraha matatu na hakuwa na nguo hata moja," amesema Mboryo.



Akimzungumzia marehemu, Mbotya  amesema enzi za uhai wake aliwahi kufanya kazi Jeshi la polisi kitengo cha upelelezi katika mikoa mbalimbali pamoja na kuwa mlinzi eneo la Ikulu ya Magogoni jijini Dar es Salaam kwa miaka mitatu katika utawala wa awamu ya kwanza Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere.

Jitihada za kumpata Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma, Gilles Muroto zinaendelea na yupo eneo la msiba Chang’ombe kunakofanyika maandalizi ya mazishi.

Gari la polisi ndilo limetumika kubeba mwili wa Bura kutoka Hospitali ya Rufaa ya Dodoma kuupeleka nyumbani kwake.



Endelea kufuatilia Mwananchi kujua kinachoendelea

Mwananchi
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad