Mzee wa Miaka 71 Akamatwa Kwa Kuipigia Simu Kampuni Mara 24,000 Akitaka Aombwe Radhi
0
December 06, 2019
Jeshi la polisi nchini Japan linamshikilia mzee mwenye umri wa miaka 71 kwa kuipigia simu kampuni moja mara 24,000 kupitia namba ya bure, akiilalamikia kuwa imekiuka mkataba kati yao.
Mwanaume huyo aliyetajwa kwa jina la Akitoshi Okamoto alifikishwa kwenye selo za polisi Novemba 26, 2019 na kufunguliwa mashtaka ya udanganyifu na usumbufu kwenye biashara, kwa mujibu wa msemaji wa polisi wa Tokyo.
Msemaji huyo wa Polisi ameiambia CNN kuwa mwanaume huyo alipiga simu mfululizo kwa kampuni ya KDDI ambayo ni moja kati ya makampuni makubwa ya simu za mkononi nchini humo; na aliwataka wafanyakazi wa kampuni hiyo kwenda nyumbani kwake kumuomba msamaha kwa kuvunja masharti ya huduma alizopaswa kupewa.
“Na mara kadhaa alikuwa akikata simu mara tu simu hiyo ilipopokewa,” msemaji huyo anakaririwa na CNN.
Kwa mujibu wa taarifa rasmi ya polisi, KDDI imeeleza kuwa ilipokea jumla ya simu 24,000 kutoka kwa mzee Okamoto tangu Mei 2017.
Hivyo, kutokana na usumbufu na kuingilia kwa kiasi kikubwa huduma za wateja, waliamua kufungua kesi Oktoba mwaka huu baada ya kuona ameongeza kasi ya kupiga simu kupitia namba ya huduma kwa wateja.
Hata hivyo, Okamoto amekana tuhuma zote dhidi yake na amewaeleza polisi kuwa yeye ndiye aliyekuwa muathirika katika sakata hilo.
Shirika la Utangazaji la Japan limeeleza kuwa mzee huyo anaamini kuwa KDDI walikiuka mkataba wake wa huduma kwa sababu hakuweza kupiga simu kwenye kipindi cha redio kwa kupitia namba ambayo ilitolewa na kituo hicho.
Kwa mujibu wa sheria za Japan, mtu yeyote anayeingilia utendaji wa biashara halali, akikutwa na hatia anaweza kufungwa hadi miaka mitatu jela.
Tags