Nyimbo 10 Zilizotikisa Bongo 2019



 MOJA kati ya mafanikio kwa msanii kwa mwaka mzima ni kutoa nyimbo ambazo zitakuwa kali, zitapigwa na kupendwa na watu wengi kwa muda mrefu.



Mwaka 2019 ndio huo unaelekea ukingoni, Risasi Vibes inakuletea orodha ya ngoma 10 zilizofanya vizuri kwa mwaka huu hususan zile ambazo zimetoka hivi karibuni na kuumaliza mwaka vizuri.



MUNGU ANAKUONA – NAY WA MITEGO

Huu wimbo Nay ameuachia Desemba Mosi mwaka huu. Ni wimbo wenye ujumbe ambao umemweka Nay kwenye ramani ya wasanii waliomalizia mwaka vizuri. Hadi mwishoni mwa wiki iliyopita, wimbo huo ulikuwa umetazamwa na wafuasi 284, 749 katika mtandao wa You Tube.



BABA LAO – DIAMOND

Kama lilivyo jina lake, wimbo huu kweli ni Baba Lao. Ni wimbo ambao uliingia sokoni Novemba 8 lakini umechezwa sana. Taarifa ikufikie tu, mpaka mwishoni mwa wiki iliyopita, tayari ulikuwa umeshatazamwa na wafuasi 7, 734, 614.

Ni wimbo ambao unaongoza kupigwa katika klabu mbalimbali pamoja na vituo mbalimbali vya redio pamoja na televisheni.



UNO – HARMONIZE

Balaa lake lilikuwa si la kitoto alipoiachia Novemba 4. Ulikubalika na unaendelea kukubalika. Kwa sasa una watazamaji 4, 230, 804. Ulitofautiana siku chache na ule wa bosi wake wa zamani Diamond lakini unaendelea kukimbiza mpaka sasa.





BUGANA –  BILLNASS

Huu ni moja ya nyimbo nzuri zilizozalishwa na kubamba mwaka huu kutoka kwa Billnass. Mkali huyo wamichano alijiongeza kwa kutia ladha ya mtoto wa Kipare, Faustina Charles ‘Nandy’ ambaye ameufanya wimbo huo uzidi kuwa mtamu.



Aliuachia Oktoba na ulifanya vizuri sana kwa mwezi huo hadi Novemba. Hadi mwishoni mwa wiki iliyopita, wimbo huo ulikuwa na wafuasi 2,051, 224 katika mtandao wa You Tube.





MSHUMAA – KIBA

Mkongwe Ally Saleh Kiba ‘Alikiba’ naye hakuachwa nyuma mwaka huu. Wimbo wake wa Mshumaa alioutoa Novemba 8, ulipata mapokeo mazuri. Ni wimbo ambao unachezeka na kama unakumbuka, aliutoa siku moja na mpinzani wake Diamond.



Kwa kiasi chake ulipigwa na unaendelea kupigwa mpaka sasa kwenye kumbi za starehe, redio pamoja na televisheni. Una wafuasi 2,629,865 huko You Tube na ni wimbo ambao unachezeka.



BADO – VANESSA

Huu ni wimbo ambao umefanya vizuri sana. Mtoto wa kike anayefanya poa kimataifa; Vanessa ameona ni vyema na haki kumshirikisha dogo kutoka pale WCB, Rayvanny. Aliuachia Oktoba 16 na mpaka sasa una wafuasi 1,646582.



Wimbo huu ni moja kati ya nyimbo ambazo zina video kali na inachezeka sana klabu za usiku. Watu wameendelea kuuchagua sana.



KIZA KINENE – NANDY

Mtoto wa Kipare mwenye sauti ya aina yake, amekuwa na rekodi nzuri ya kuachia nyimbo kali. Kiza Kinene ni kati ya ngoma zake kali za mwaka huu na imefanya vizuri sana kunako anga la Bongo Fleva. Wimbo huu aliuachia Septemba 6 lakini hadi sasa unaendelea kukimbiza.



Amewashirikisha Sauti Sol kutoka Kenya na kujikusanyia wafuasi 3,117, 953. Mbali na ngoma hiyo, Nandy amekuwa akifanya vizuri tangu aanze muziki miaka michache tu iliyopita.





TETEMA – RAYVANNY

Hili goma tangu limetoka Februari, mpaka sasa bado ni tamu tu kulisikiliza. Lilipigwa na linaendelea kupigwa sana kwenye redio na televisheni. Bwa’mdogo kutoka Wasafi Classic Baby (WCB) aliutendea haki wimbo huo alioshirikiana na Diamond.



Limekuwa kama wimbo wa taifa. Umepigwa sana wimbo huu kama ilivyokuwa kwa Kwangwaru. Ni wimbo ambao hauishi hamu, kila ukipigwa bado unatamani kuusikiliza. Una wafuasi 34, 431,954 mpaka sasa!



WE ENDELEA TU – MWANAFA

Mara nyingi ni nadra sana kuona nyimbo za Hip Hop zinakaa kwa muda mrefu kwenye chati lakini hili limewezekana kwa mkali Hamisi Mwinjuma ‘MwanaFA’. Wimbo wake huo umependwa sana kwenye vyombo vya habari hususan redio na televisheni licha ya kuwa hauna wafuasi wengi sana You Tube.



Wimbo huo una wafuasi 932, 212 lakini unapokwenda kwenye kumbi za starehe na maeneo mbalimbali ya hadhara, wimbo huo unachezwa sana.



ANAITWA ROMA – ROMA

Huu nao ni miongoni mwa nyimbo ambazo zimepigwa sana mwaka huu. Roma aliuachia Novemba 14 akiwa safarini nje ya nchi. Uliwashika watu wengi sana kutokana na kuwa na mashairi yenye ukakasi hususan kwa viongozi wa Serikali kiasi cha watu kudhani utafungiwa lakini haikuwa hivyo.



Wimbo huo una wafuasi 914, 827. Wimbo huo ni mwendelezo wa ngoma kali za Roma ikiwemo ile ya Kijiwe Nongwa ambao wamefanya na Stamina kupitia umoja wao wanaouita Rostam. Wimbo huo una wafuasi 2,035,942. Wimbo huo wamemshirikisha Nay wa Mitego.

Makala: ERICK EVARIST
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad