MAHAKAMA ya Embu nchini Kenya, imemfunga afisa mmoja wa polisi miaka 20 baada ya kupatikana na hatia ya kuwaua watu 10.
Peter Karanja anaarifiwa kutekeleza mauaji hayo akiwa kwenye harakati za kumsaka mwanamke aliyedaiwa kumuambukiza Virusi Vya Ukimwi.
Alishtakiwa Novemba 6, mwaka huu, ambapo mahakama ilielezwa kuwa mtuhumiwa huyo alitekeleza mauaji ya watu hao kumi nje ya klabu tatu tofauti katika mji Siakago Kaunti ya Embu nchini Kenya.
Hata hivyo, Afisa huyo alikana mashtaka hayo aliposhtakiwa lakini ushahidi ulitosha kumtia hatiani. Karanja alishtakiwa kwa kumuua Anthony Mwaniki, Frida Ng’endo, Kenwin Muthomi, Agostino Kinyua na George Ng’ang’a.
Wengine ni Domisiano Muchira, Ephantus Munyi, Rachel Muthoni, Wilfred Gitonga na Fredrick Okwako. Upande wa mashtaka ulikuwa na mashahidi 27 na ushahidi uliotolewa ulikuwa ni vifaa vilivyotumika katika mauaji hayo.
Ilielezwa mahakamani kuwa afisa huyo wa kitengo cha polisi wa utawala, alitoka katika eneo lake la kazi na kuelekea katika klabu ya New Coconut kumsaka mpenzi wake. Alipofika aliwapiga risasi na kuwaua watu watatu kabla ya kuelekea katika Waiyaki Bar ambapo alimpiga risasi na kumuua mtu mwingine.
Baada ya hapo alielekea katika klabu ya Tha Shrek ambapo aliwaua watu wengine wanne. Maafisa wenzake wawili waliokuwa wameitwa kudhibiti hali, pia aliwamiminia risasi. Baadaye afisa huyo alijaribu kujipiga risasi, lakini zilikuwa zimekwisha na hivyo kutiwa mbaroni.