RASMI Niyonzima Mali ya Yanga, Kutua Nchini


RASMI uongozi wa Yanga umethibitisha kuwa unakamilisha usajili wa kiungo mchezeshaji fundi wa AS Kigali ya Rwanda, Haruna Niyonzima ambaye siku yoyote kuanzia leo Jumatano atatua nchini kufanikisha usajili wake.



Niyonzima aliwahi kuichezea Yanga kwa mafanikio makubwa akichukua mataji matatu mfululizo ya Ligi Kuu Bara huku akibeba Kombe la Kagame na Kombe la FA.



Kwa mujibu wa taarifa ambazo imezipata Championi Jumatano, uongozi wa Yanga umeshafikia makubaliano mazuri ambayo yana asilimia 100 na kiungo huyo.

Mwenyekiti wa Yanga, Mshindo Msolla akizungumza na viongozi wa Baraza la Wazee la timu hiyo juzi alisema kuwa wapo kwenye mchakato wa mwisho kabisa wa kumchukua kiungo huyo mahiri.


Mtoa taarifa aliliambia Championi kuwa wazee walishangilia sana baada ya kuelezwa kuwa Niyonzima anarejea tena Jangwani hali ambayo inaonyesha kuwa ni kipenzi chao.



“Katika kikao tulichofanya kati yetu sisi Wazee wa Yanga na viongozi, mengi yamejadiliwa na kati ya hayo ni hili zoezi la usajili linaloendelea ni baada ya viongozi kututhibitishia mengi mazuri lakini kati ya hayo ni hili la kumrejesha Niyonzima.



“Kiukweli sisi Wazee wa Yanga tulifurahi sana, ipo wazi Niyonzima ni kati ya viungo bora Afrika Mashariki na Kati, hatukuwa na kiungo mchezeshaji mwenye uwezo mkubwa wa kumiliki mpira na kupiga pasi za mabao.



“Hivyo kurejea kwake kumetufanya sisi wazee kupata morali ya kwenda uwanjani kuiangalia timu yetu itakapokuwa ikicheza mechi zake za ligi ikiwemo ile na watani wetu wa jadi, Simba,” alisema mtoa taarifa huyo.



Msolla hivi karibuni alithibitisha kufanya mazungumzo na Niyonzima huku akisema kuwa: “Niyonzima ni kati ya wachezaji waliopo kwenye mipango yetu na kama mipango ikikaa sawa, basi atajiunga na Yanga katika dirisha dogo.”



Imeelezwa kuwa timu hiyo imemwandalia Niyonzima mkataba wa miaka miwili, wakiamini kuwa atakuwa msaada mkubwa kwao kwenye mechi dhidi ya Simba, Januari 4.

Pia kiungo huyo karibuni alikiri kufanya mazungumzo na Yanga na kuwa anatamani kurejea klabuni hapo.

Stori na Wilbert Molandi, Dar es Salaam
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad