Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam Mhe. Paul Makonda leo Disemba 18 ametembelea na kukagua miundombinu iliyoharibiwa na Mvua ambapo amewahakikishia Wananchi kuwa Serikali ipo katika hatua ya kukarabati miundombinu yote iliyoharibiwa na Mvua ili irudi katika hali ya kawaida na kuwaondolea wananchi kero.
RC Makonda amesema Serikali imejitaidi kwa kiasi kikubwa Kujenga miundombinu ya kupitisha maji ya Mvua ikiwemo upanuzi wa Mito, Madaraja na Mifereji lakini kinachotokea ni tabia chafu ya baadhi ya Wananchi kutupa taka kwenye miundombinu hiyo jambo linalosababisha maji kushindwa kupita kwenye njia yake na kusababisha mafuriko.
Aidha RC Makonda amewataka wananchi waliojenga na wanaoishi katika maeneo hatarishi kuhakikisha wanahama kwakuwa Mvua bado zitaendelea kunyesha kwa Mujibu wa Taarifa iliyotolewa na Mamlaka ya Hali ya Hewa.
Hata hivyo RC Makonda amesema Serikali kwa sasa inaendelea kutekeleza miradi mikubwa Ujenzi wa Mito na Mifereji kwa lengo la kupunguza kero mafuriko kwa wawananchi ambapo kwa Wilaya ya Ilala kuna ujenzi wa Mito yenye urefu wa Km 16, Temeke Km 14 na Kinondoni Km 8 ili maji yaende moja kwa moja Baharini.
Pamoja na hayo RC Makonda amesema miongoni mwa miradi hiyo ni pamoja na Ujenzi na Upanuzi wa Mto Ng'ombe, Mto Msimbazi, Ujenzi wa Daraja la Juu eneo la Jangwani pamoja na Maboresho ya eneo hilo ili liweze kutumika kwa shughuli za utalii wa Boti.