Sababu bendera za Chadema Kushushwa Hii Hapa
0
December 18, 2019
Dar es Salaam. Mkurugenzi wa Manispaa ya Ubungo, Beatrice Dominic amesema bendera za Chadema zilizowekwa katika barabara ya Sam Nujoma, jijini Dar es Salaam zimeshushwa kwa sababu chama hicho hakikuomba kibali.
Amesema kama wangeomba kibali kabla ya kuziweka zisingeshushwa.
Beatrice ameeleza hayo leo Jumatano Desemba 18, 2019 baada ya kupita saa 24 tangu alipoliagiza Jeshi la polisi kuziondoa bendera hizo zilizowekwa karibu na ukumbi wa Mlimani City unakofanyika mkutano mkuu wa chama hicho leo. Polisi waliondoa bendera hizo jana saa 4 usiku.
“Eneo lolote linalohudumiwa na manispaa kwa maana ya usafi, kupanda maua litatumika baada ya kupewa kibali na manispaa.”
“Uongozi wa Chadema ulitakiwa kuomba kibali kwa mkurugenzi lakini hawakufanya hivyo na nilipowaandikia barua wazishushe walikaidi agizo ndio maana tulitumia njia nyingine,” amesema Beatrice.
Bendera hizo ziliwekwa kuanzia eneo la Superstar hadi eneo la ukumbi huo, karibu na kanisa na Full Gospel Bible Fellowship (FGBF).
Leo Mwananchi limeshuhudia eneo hilo likiwa halina bendera hizo ambazo wakati zikishushwa jana, polisi walilazimika kutumia mabomu ya machozi kuwatawanya baadhi ya watu.
Kabla ya kuagiza polisi kushusha bendera hizo, mkurugenzi huyo alikiandikia barua chama hicho kukipa saa mbili kuondoa bendera zake.
Katika barua hiyo ya Jumanne Desemba 17, 2019 kwenda kwa katibu mkuu wa Chadema, Dk Vicent Mashinji ambayo Mwananchi imeona, mkurugenzi huyo amesema manispaa ya Ubungo ndio inayoihudumia barabara hiyo inashangazwa kuona bendera za chama hicho zikiwa kwenye bustani.
Dominic amesema bendera zimewekwa kama matangazo kinyume na utaratibu wa kibali.
"Kwa barua hii nakutaarifu kuwa unatakiwa uondoe bendera hizo ndani ya muda wa saa mbili baada ya kupokea barua hii. Agizo hii lisipotekelezeka bendera hizo zitaondolewa kwa utaratibu mwingine," inasomeka sehemu ya barua hiyo.
Hata hivyo Meya wa Ubungo ambaye pia ni mjumbe wa kamati kuu ya Chadema, Boniface Jacob alipoulizwa kuhusu agizo hilo la mkurugenzi amesema, “bendera hizo haziondolewi kwa sababu Chadema tuna haki ya kutumia maeneo ya wazi ya umma kama vyama vingine vya siasa kwa mujibu wa sheria.”
Mwananchi
Tags