Sababu zatajwa Wasafiri wa TRENI Kushindwa Kukata Tiketi Kimtandao


Dar es Salaam. Kutokuwapo kwa upatikanaji wa uhakika wa mabehewa ya kusafiri, kumeelezwa kuwa chanzo cha abiria wa usafiri wa treni kushindwa kukata tiketi kwa njia ya mitandao ya simu.

Hayo yameelezwa leo Jumatatu Desemba 23, 2019 na Ofisa Mtendaji Mkuu wa Serikali Mtandao, Dk Jabir Bakari katika mkutano kati ya bodi, menejimenti na Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Isaack Kamwelwe kujadili namna ya kutatua changamoto mbalimbali za usafiri huo.

Dk Bakari amesema kwa namna mfumo wa kompyuta ulivyowekwa ni lazima kuwepo kwa usafiri wa uhakika katika ratiba ya siku treni itakaposafiri ili kuwaondolewa adha wasafiri kukata tiketi.

“Hii ni pamoja na kujua siti atakayokaa, behewa na muda wa kuondoka, lakini kwa bahati mbaya katika usafiri huu kuna wakati mabehewa yanapunguzwa kutokana na hitilafu mbalimbali jambo litakalochanganya mfumo.”

“Pia haipendezi mtu anakata tiketi halafu anafika stesheni hakuna usafiri wakati fedha yake imeshakatwa na kurudishiwa inachukua muda kutokana na kuhusisha taasisi tofauti katika makato hayo, hivyo ni lazima tujidhihirishe kabla ya kuingia humo na kuepuka kuwasababishia adha wasafiri,” amesema Dk Bakari

“Jambo hili tumeweza kufanikiwa zaidi kwenye usafiri wa ndege ambapo mtu anakata tiketi akiwa nyumbani kwake kwa kuwa usafiri huu ni wa uhakika wanapokuambia ndege itasafiri siku na muda fulani.”


Ofisa mtendaji mkuu huyo amesema, “lakini kwa treni bado, kwani wanaweza wakasema mabehewa nane yatasafiri lakini isiwe hivyo ndiyo maana inakuwa ngumu kuwaingiza katika mfumo huo.

Awali, Waziri  Kamwelwe amesema wanatamani wafikie huko lakini wanachelewa kutokana na baadhi ya wafanyakazi kufanya kazi kwa mazoea.

“Kuna baadhi ya wafanyakazi hawataki kubadilika, wamezoea kukusanya fedha wanazokata za nauli na baadaye kuzibeba kupeleka benki, halafu huko ndiyo wanafanya yale mambo yao ya kuiibia Serikali, lakini tunakoelekea hili litaisha na ni baada ya kuwa na mabehewa ya kutosha.”

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Reli Tanzania  (TRC), Masanja Kadogosa amesema wana mpango wa kuongeza mabehewa zaidi ya 40 ya kisasa ambayo wanaamini kwa namna yatakavyokuwa yametengenezwa yatakidhi ukataji tiketi huo wa kidigitali.
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad