Serikali Kuongeza Uzalishaji wa Majongoo Bahari
0
December 16, 2019
Serikali imesema inahakikisha sera yake ya kuhamasisha wananchi kufuga samaki , kaa, Majongoo bahari na kambakochi, inatekelezwa kote nchini ili kutosheleza mahitaji ya soko pamoja na kukuza pato la taifa na mtu mmoja mmoja.
Hayo yamebainishwa na Naibu waziri wa Mifugo na uvuvi, Abdallah Ulega wakati akifungua tawi la wakala wa Elimu na mafunzo ya Uvuvi (FETA), kampasi ya Mkikindani mkoani Mtwara.
Ulenga ameagiza FETA kwa kushirikiana na idara ya ukuzaji viumbe kwenye maji kutoka katika wizara hiyo, kuandaa mitaala ya ufugaji viumbe kwenye maji wakiwemo Samaki, Kaa, majongoo bahari na Kambakochi kwaajili ya wananchi wa ukanda wa Pwani ili waweze kuongeza vipato vyao kupitia fursa ya ufugaji.
Pia ameagiza uundwaji wa vikundi vya uzalishaji kaa, Kambakochi, majongoo bahari pamoja na wazalishaji wa zao la mwani ili iwe rahisi kwa vikundi hivyo kutambulika rasmi pindi mazao yao yanapo hitajika sokoni.
Mkurugenzi wa mafunzo kutoka FETA, Ambakisye Simtoe amesema wamejiandaa kuzalisha wagani kwaajili ya kuendeleza na kukuza tasnia ya uvuvi nchini pamoja na kununua mashine ya kuzalisha vifaranga bora.
Ikumbukwe kuwa kwa mujibu wa takwimu kutoka wizara ya mifugo na uvuvi mahitaji ya soko la samaki nchini ni tani 700, 000 hadi 800,000 kwa mwaka huku uzalishaji ukiwa wastani wa tani 400,000 hadi 450, 000.
Tags