Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Isaack Kamwelwe, amesema uendeshaji wa bandari nchini hautarudishwa nyuma tena kama ilivyokuwa imefanywa na mafisadi.
Kamwelwe alitoa kauli hiyo alipotembelea Bandari za Bukoba na Kemondo zilizoko mkoani Kagera.
Alisema baada ya bandari nyingi kusitisha shughuli zake kwa kipindi kirefu kulikosababishwa na matatizo mbalimbali, wakiwamo mafisadi waliokuwa wakipenda kujinufaisha wenyewe, serikali imeanza mkakati wa kuzifufua na kuboresha zaidi zinazofanya kazi.
"Tunafanya maboresho katika bandari zetu zote, tunataka turudishe huduma kwa kasi kubwa hata kwa zile ambazo zilikuwa zimesitisha huduma zake, ulifanyika uzembe, waliturudisha nyuma mafisadi, lakini tumefanikiwa kunyanyuka, hatutakubali kurudishwa nyuma tena walikokuwa wametufikisha.
"Juhudi zinazofanywa na Rais John Magufuli za kukarabati bandari na meli, meli zinabadilika zinakuwa mpya, hususani meli ya Mv Victoria na Mv Butiama ambazo mpaka Aprili mwakani zitaanza kufanya kazi.
"Nimekuja kukagua maboresho haya yanayofanyika, kazi inaendelea vizuri na ninaipongeza Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari (TPA) kwa kazi kubwa wanayofanya katika uboreshaji huu wa bandari.
"Usafiri wetu wa raha uliopotea kwa miaka mingi, sasa unarudi, Mv Victoria sasa itatoa huduma zake katika ziwa hili na itafika Uganda mpaka Kenya, tunatarajia wananchi wataondokana na shida ya usafiri ambayo imekuwapo kwa muda mrefu," alisema.
Akizungumzia maboresho yanayofanyika katika reli, Kamwelwe alisema kwa sasa serikali imepanga kufufua usafiri huo kuwa kama wa barabara.
Alisema wako kwenye mpango wa kuandika waraka ambao wataufikisha kwenye baraza la mawaziri na kisha bungeni ili kuruhusu wafanyabiashara kununua mabehewa ya treni kwa ajili ya kusafirishia mizigo yao.
"Wafanyabiashara watakuwa wananunua behewa kwa ajili ya mizigo yao, halafu sisi tutakuwa tunawachaji gharama ya kutumia reli yetu, lengo ni kutaka sekta hii ifike mbali na itumike kwa kiwango kikubwa kuongeza uchumi wa nchi," alisema.