TIMU ya Simba wameitumia salamu Yanga baada ya kuichapa KMC mabao 2-0 kwenye Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam leo Desemba 28, 2019.
Mabao ya Simba yamefungwa na Deo Kanda dakika ya 46 na Mbrazil Gerson Fraga katika dakika 90 yametosha kuipa Simba pointi tatu na kuendelea kujikita kileleni mwa ligi kwa pointi 31 na kujiweka vizuri kuelekea katika mchezo wa watani wa jadi dhidi ya Yanga utakaofanyika Jumamosi ijayo.
Ushindi huo unamfanya kocha mpya wa Simba, Sven kuendeleza rekodi ya ushindi katika michezo mitatu aliyoiongoza timu tangu alipochukua mikoba Partick Aussems.
Katika mchezo huo KMC iliyocheza kwa kujilinda vizuri katika kipindi cha kwanza ilipoteza uelekea mwanzoni mwa kipindi cha pili kwa kuruhusu bao la mapema la Deo Kanda aliyemalizia kwa shuti la chini krosi ya Hassan Dilunga.
Baada ya bao hilo Simba walichangamka na kuongeza mashambulizi, lakini KMC ilionekana kurudi mchezoni na kuongeza umakini katika kujilinda chini ya kipa wake Jonathan Nahimana.
Kiungo Mbrazili Gerson Fraga alifunga bao lake kwanza la Ligi Kuu akiwa na Simba kwa kuunganisha krosi Francis Kahata kwa shuti kali la chini akiwa nje ya eneo 18 katika dakika ya 90+3 likiwa ni bao la pili la Simba.
PICHA NA MUSA MATEJA, GPL