Sudan Kuwalipa Waathiriwa wa Mabomu ya Osama, Kenya na Tanzania ya Mwaka 1998
0
December 11, 2019
Waziri mkuu mpya wa Sudan Abdalla Hamdok, ameahidi kwamba taifa lake hivi karibuni litawafidia takriban dola bilioni 6 waathiriwa wa mkasa wa mabomu nchini Kenya na Tanzania katika balozi za Marekani za 1998 mjini Nairobi na Dar es Salaam.
Amenukuliwa na gazeti moja nchi Marekani akisema ”Tulichukua jukumu la kuangazia madai hayo na kuafikia makubaliano”,
Hamdok ametoa ahadi hiyo wakati wa ziara yake ya kwanza nchini Marekani ambapo alitaka Sudan kuondolewa katika idadi ya mataifa yalioorodheshwa na Marekani kwamba yanaficha magaidi.
Takriban familia 570 za wafanyakazi wa balozi za Marekani na wanakandarasi waliouawa katika mashambilio pacha yaliotekelezwa na kundi la al Qaeda mjini Nairobi na Dar es Salaam wanatarajiwa kufidiwa.
224 walifariki katika mashambulio hayo pacha- 214 mjini Nairobi na 10 Dar es Salaam.
Mahakama za Marekani zimeiwajibisha Sudan kulipa fidia ya $5.9 bilioni kwa watu hao kwa kuwa ilihusika kumficha kiongozi wa kundi la al-Qaeda Osama bin Laden wakati alipokuwa akipanga njama za kutekeleza mashambulio hayo.
Waziri Mkuu Hamdok aliateuliwa mwezi Agosti kufuatia maandamano dhidi ya serikali ambayo yalimng’atua madarakani aliyekuwa Rais wa taifa hilo Omar al- Bashir.
Kiongozi huyoo mpya ameahidi kufanya mabadiliko katika sera za ndani za taifa hilo pamoja na zile za kimataifa.
Tags