Sumaye Awashangaza Chadema...Wamepoteza Lulu Mchangani


Hatua ya Frederick Sumaye, aliyekuwa Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia (Chadema), Kanda ya Pwani kuangushwa kwenye uchaguzi wa kanda hiyo, imemshtua Prof. Abdallah Safari, makamu mwenyekiti wa chama hicho.

Akizungumza na Mwanahalisi Prof. Safari ameonesha kushangazwa baada ya Sumaye kuangushwa kwenye uchaguzi huo uliofanyika tarehe 28 Novemba 2019.

“Ninavyomjua Sumaye na jinsi alivyo lulu kwenye chama hiki, Chadema kimepoteza lulu kwenye kanda hiyo. Sumaye ni muungwana, mwadilifu na mwenye uwezo mkubwa kwenye uongozi.

“Nawatahadharisha Chadema pia nawaonya kwamba wanacheza na lulu. Naona wanazungumzia demokrasia lakini nashangaa kwanini hawawajui watu wenye weledi, uwezo mkubwa na mawazo chanya katika kuongoza. Sielewi kwanini hili halionekani ndani ya chama,” amesema Prof. Safari.

Prof. Safari ambaye ni mwanasheria mkongwe amesema, anatarajia kuendelea na maisha yake baada ya kukabidhi nafasi yake ya umakamu mwenyekiti kwa viongozi wajao.

Sisty Nyahoza, Naibu Msajili katika Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa nchini, ametahadharisha Chadema kuzingatia kanuni za uchaguzi.

Akizungumza na chombo kimoja cha habari nchini, Nyahoza kwa niaba ya msajili wa vyama amesema, ofisi yake haitaona tabu kutotambua viongozi watakaochaguliwa pale itapojiridhisha kama mbinu hasi zilitumika.

Tarehe 18 Novemba 2019, chama hicho pamoja na mambo mengine, kinatarajiwa kupata viongozi wake wakuu akiwemo mwenyekiti Taifa.

Chanzo: Mwanahalisi
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad