Dk Mahanga Achambua Kupigwa CHINI Kwa Sumaye..."Uenyekiti Taifa Ndiyo Umemponza"
0
December 01, 2019
Ni mawazo yangu kwamba Mhe. Frederick Sumaye na wapiga kura wa Baraza la Uongozi la Kanda ya Pwani wote wanaweza kuwa na sehemu yao ya lawama katika sakata la Sumaye kunyimwa kura za kuwa Mwenyekiti wa Kanda hiyo.
Kwa wapiga kura sehemu yao ya lawama inaweza kuonekana kwamba iko wazi zaidi wakati kwa upande wa Sumaye mtu anaweza kuona hastahili lawama, lakini kumbe anastahili lawama ambazo lazima uziangalie kwa jicho la tatu la kisiasa kuweza kuzitambua vizuri. Nitafafanua
Kwa wapiga kura lawama zinaonekana ziko wazi kwa sababu wamemwadhibu Sumaye kwenye sanduku la kura kwa sababu tu ya nia yake ya kutaka kutekeleza haki yake ya kikatiba na demokrasia ya kugombea nafasi ya Uenyekiti wa Chadema Taifa. Ni vigumu kuona ni sababu gani nzuri zilizowafanya wapiga kura walio wengi wa Kanda ya Pwani kumkataa Sumaye kwenye nafasi ya Uenyekiti wa Kanda ya Pwani kwa kumpigia kura nyingi za HAPANA, tena baada ya kumwachia agombee nafasi hiyo peke yake bila mpinzani. Shida imetoka wapi ghafla? Ni rahisi kusema hakukuwa na sababu nzuri bali ni ile tu azma yake ya kugombea pia nafasi ya Uenyekiti Taifa ndiyo iliyomponza. Kama kugombea nafasi hiyo ya Uenyekiti wa Taifa ni haki ya kidemokrasia ya mwanachama yeyote, kwanini wapiga kura wa Kanda ya Pwani wakaamua kumwadhibu Sumaye kwa hili?
Nataka nieleze mazingira ambayo watu wanatakiwa wayaone kwa jicho la tatu la kisiasa kabla ya kuwapa lawama zote wapiga kura wa Kanda ya Pwani waliompigia kura za HAPANA Sumaye. Ni imani yangu pia kwamba Sumaye naye hakuangalia mazingira haya kwa umakini wa kisiasa hasa kwa mwanasiasa mkubwa na mkongwe kama yeye. Mazingira haya ni ya muda mrefu sasa ingawa mengine yamejitokeza kuelekea uchaguzi wa Kanda na siku yenyewe ya uchaguzi wa Kanda ya Pwani ambayo hayakuwa rafiki kwa upande wa Sumaye na yeye hakuyang’amua kabla kwa jicho kali la kisiasa. Baadhi ya mazingira haya toka kabla ya uchaguzi huu na mpaka wajumbe kupiga kura Kanda ya Pwani ni kama yafuatayo:
1. Ukifuatilia mjadala na mchakato wa Uchaguzi wa Chadema ngazi ya Taifa mwaka huu, hata kabla haujatangazwa rasmi, kumekuwepo na hisia kali sana miongoni mwa wanachama wa Chadema, wanachama wa vyama vingine, wananchi wa kawaida na hata ndani ya vyombo vya Serikali vikiwemo vya usalama kuhusu kwa nini Mbowe
bado anafaa au hafai kuendelea kuwa mwenyekiti wa Chadema. Mijadala hii imefanyika kwa hisia kali kwenye mitandao ya kijamii na kwenye mijadala rasmi na isiyo rasmi