Tanasha Afungasha Virago, Asepa Kwao, Mama Dangote Atajwa
0
December 03, 2019
AMKENI… amkeni… amkeni… njooni huku! Habari ikufikie kuwa, mzazi mwenza wa staa wa Bongo Fleva, Nasibu Abdul ‘Diamond Platnumz’, Tanasha Donna Oketch, amefungasha virago jijini Dar na kurejea nyumbani kwao nchini Kenya, Gazeti la IJUMAA WIKIENDA linakupa zaidi.
Habari zinaeleza kuwa, baada ya kumaliza sherehe ya 40 ya kumtoa mwanaye Naseeb Junior iliyofanyika nyumbani kwa mama mzazi wa Diamond au Mondi, Sanura Kassim ‘Bi Sandra’, Madale- Tegeta jijini Dar, ndipo Tanasha akafungasha kila kilicho chake na kumbeba mwanaye kisha akasepa zake.
KWA NINI?
Chanzo makini kililieleza Gazeti la Ijumaa Wikienda kuwa, kuondoka kwa Tanasha siyo kwa mazuri, bali kuna sababu kubwa ambayo ni kutofautiana na mamamkwe wake; yaani Mama Mondi au Mama Dangote.
Kiliendelea kueleza kuwa, wawili hao walitofautiana siku chache kabla ya 40 ya Naseeb na ndiyo maana kabla sherehe haijafanyika, mama Mondi alisema haipo ilhali mkwewe Tanasha akisema ipo kwa kuweka matangazo kwenye Mtandao wa Kijamii wa Instagram.
“Unajua mama Mondi na Tanasha walitofautiana hata kabla ya sherehe ya mtoto, ndiyo maana kama mlifuatilia vizuri kwenye sherehe walikuwa hawako karibu kama mtu na mkwewe.
“Hakuna sehemu yoyote ambayo mama Dangote au Tanasha anambeba mtoto na kumpa mamamkwe; yaani wanapishana tu ndiyo maana hata muda mwingi Mondi ndiye aliyekuwa akimfuta jasho usoni Tanasha. Muda mwingi Mondi ndiye aliyekuwa bize na mzazi mwenzake,” kilitiririka chanzo.
SOSI NI HII
Chanzo hicho kiliendelea kueleza kuwa, sosi ya kutofautiana kwao ni baada ya mama Mondi kuwapeleka wageni wake nyumbani kwa Tanasha, lakini badala ya kuwapokea akaenda kujifungia chumbani kwake na kulala.
“Mama Mondi alitembelewa na wageni wake nyumbani kwa Tanasha wanapoishi na Mondi, Mbezi Beach Dar, maana ndipo alipokuwa kwa ajili ya kumsaidia mkwewe, lakini cha ajabu alipoitwa na kuambiwa kuna wageni, mwanamama huyo alijifungia chumbani na mwanaye.
“Yaani alijifungia na kulala hata hakumtoa mtoto ili wageni wamuone, jambo ambalo lilimuudhi mama Mondi hadi kwenye shughuli ya mtoto huyo wakawa hawako sawa mpaka alipoamua kufungasha virago na kuondoka,” kilisema chanzo hicho.
ASHINDWA KUMUAGA
Kutokana na kutofautiana huko, chanzo hicho cha habari kinaeleza kuwa, licha ya kuwa bado mama Mondi yupo nyumbani hapo, Tanasha hakumuaga kuwa anakwenda kwao.
“Unaambiwa hata wakati Tanasha anaondoka kurudi kwao (Kenya), hakumuaga mama Mondi, alichofanya ni kumchukua mwanaye na vitu vyake na kuondoka; yaani mambo yamekorogeka balaa, sijui kama atarudi tena,” kilieleza chanzo.
MAMA MONDI SASA
Baada ya kupata habari kutoka kwa chanzo hicho, IJUMAA WIKIENDA lilimbana mama Mondi ambaye alifunguka mazito kama ifuatavyo;
Ijumaa Wikienda: Tumesikia mkweo Tanasha ameondoka, kuna ukweli?
Mama Mondi: Ni kweli ameondoka.
Ijumaa Wikienda: Kuna habari kuwa mlikuwa na mgogoro na ni baada ya wewe kwenda na wageni wako ili wamuone mtoto, lakini Tanasha akaenda kujifungia chumbani na kulala, hili likoje?
Mama Mondi: Hizo habari sizijui, huo ni uongo na umbea tu.
Ijumaa Wikienda: Lakini hata kwenye 40 ya mjukuu wako, Naseeb JR mlikuwa mnakwepana na sababu inatajwa ni hiyohiyo, vipi hili likoje?
Mama Mondi: Mlitaka tufuatane kila sehemu jamani? Watu waache manenomaneno.
Ijumaa Wikienda: Kuna madai kuwa Tanasha ameondoka hajakuaga, ni kweli?
Mama Mondi: Siyo kweli, ataondokaje bila kuniaga wakati mimi ndiye ninakaa naye siku zote tangu hajajifungua mpaka sasa?
Ijumaa Wikienda: Kama Tanasha hajaondoka kwa ubaya, je, atarudi lini?
Mama Mondi: Sijui, hilo mnaweza kwenda Kenya mkamuulize mwenyewe.
Ijumaa Wikienda: Umesharudi nyumbani kwako, Madale kutoka kwa Tanasha Mbezi-Beach?
Mama Mondi: Sijarudi maana siwezi kuiacha nyumba bila mtu kwa sababu Mondi amesafiri, yuko Cameroon kwa ajili ya shoo.
KWA MAMA MONDI HAISHINDIKANI
Baadhi ya wachambuzi wa habari za burudani walilieleza gazeti hili kwamba, kwa mama Mondi haishindikani kukorofishana na Tanasha kwani ilishatokea hivyo wakati Mondi akiwa na Zarinah Hassan ‘Zari The Boss Lady’, Hamisa Mobeto na hata Wema Isaac Sepetu.
Stori: Gladness Mallya, Dar
Tags