Treni la Platinumz KIGOMA,Harmonize Ajigharamie


By Luqman Maloto na Dk Levy
DESEMBA 31, Diamond Platnumz ameamua kuuaga mwaka 2019 nyumbani kwao, Kigoma. Listi ni ndeefu, hata waliohama nao wamo, lakini mbona Harmonize hatajwi? Kule Yanga na Simba, mambo hayajawahi kuisha. Wabunge wa kitaa, Luqman Maloto na Dk Levy wanaishiwaje msimu huu wa sikukuu.

LUQMAN: Eti kati ya Gharib wa GSM na MO, nani ana mzigo mkubwa? Naona hizi siku mbili mashabiki wa Yanga wanamtukuza Gharib wanasema ndiye tajiri, MO hamna kitu.

DK LEVY: Gharib ana pesa mpaka nyingine zipo kwenye foleni. Yaani akaunti yake imejaa kwa hiyo pesa zingine zimeambiwa zisubiri kwanza. Ujue GSM wanaweza kununua bahari ya Hindi, samaki na mikoko yake. Acha kumfananisha tajiri Gharib na MO.

LUQMAN: Akili ya kishirikina hiyo wewe. Pesa za MO zipo kwenye rekodi za dunia. Waliosema Jeff Bezos ndiye tajiri namba moja duniani akifuatiwa na Bill Gates na Warren Buffett, ndio haohao waliomtamka MO kuwa bilionea janki Afrika na ana mkwanja mrefu kuliko wote Tanzania. MO sio wa kuzungumzwa kwa sauti ya puani kama hiyo yako.

DK LEVY: Pimbi wewe. Tutusa wewe. Zomboko wewe. Kengemaji wewe. Mbumbumbu wewe. Hayawani wewe. MO alikuwa tajiri kijana Afrika miaka mitatu iliyopita. Tena alishindana peke yake kwa kuwa wenzake walikosea kujaza fomu kama wagombea wa upinzani uchaguzi serikali za mitaa.

LUQMAN: Mkitaka kuishabikia Yanga na kumpa moyo Gharib, mnatakiwa kutumia maneno mengine sio kumponda MO. Unakuta Gharib mwenyewe role model wake ni MO, hapo lazima awaone hamnazo. MO bilionea. MO mjanja. MO mtoto wa mjini. MO mtu wa watu. Si unajua MO ma-eneji? MO nishati.

Pia Soma
HISIA ZANGU : Tunakaribishwa tena katika shoo ya Niyonzima
HISIA ZANGU : Tunakaribishwa tena katika shoo ya Niyonzima
Straika Gor Mahia aigawa Yanga
Straika Gor Mahia aigawa Yanga
Yanga yabanwa na vibonde
Yanga yabanwa na vibonde
Kocha Simba anataka mashine moja
Kocha Simba anataka mashine moja
ADVERTISEMENT
DK LEVY: Tajiri gani marafiki zake MwanaFA, Prof Jay, Haji Manara, Salama Jabir, Diamond na Ommy Dimpoz? Tajiri gani anazidiwa ulinzi na Harmonize?

LUQMAN: Na huyo ndiye MO, mtu wa watu. Habagui. Hana mbwembwe. Angetaka angelindwa kuliko Mayweather, maana MO ana mkwanja mrefu kuliko Mayweather Jr. Sasa ule ulinzi wa shoo wa Harmonize na Diamond ndio unaita ulinzi? Mimi mwenyewe nikiwa na pesa kama MO napenda niwe mtu wa watu kama yeye. Inaonekana ulivyo mtu wa shobo, MO akikunyofolea kabilioni kamoja unaweza kutupanda kichwani.

DK LEVY: Mtu wa watu au mtu wa Simba? Unajua kama Harmonize ameengia kwa steji na gari? Ila kwa kuwa wewe sotoka sahabiki sana wa WCB utapinga. Maana hamtaki kuamini kuwa mmefunikwa sana hivi sasa. Namba moja Konde Boy. Namba mbili Konde Boy. Namba tatu Konde Boy. Kuanzia namba nne ndo anza kuhesabu kunguru wako wengine. Nchi hii mwanamuziki ni Konde Boy tuuu. Kwanza anaipenda Yanga.

LUQMAN: Mambo ya kizamaaani, Ally Choki alishaingia stejini na tingatinga. Pale Diamond Jubelee katika uzinduzi wa Mtaa wa Kwanza, aliingia na Hammer. Rayvanny kwenye Wasafi Festival aliingia na Double Coaster halafu akapiga shoo juu ya Coaster na Diamond Platnumz jukwaani, Posta nzima ikatetema. Dk Levy tetema ooh mama tetema, Harmonize tetema, ooh mama tetema. Hivi wewe wa wapi? Unasifia visivyostahili aisee.

DK LEVY: Hao walitegemea kiki ya Wema miaka yote. Konde Boy hana muda huo. Na kama angetumia kiki ya madem angekimbiza dunia nzima. Kwa sababu anatoka na mzungu tofauti na hao wanaotoka na madem wa Mwananyamala, Kampala, Mombasa na Kibera Nairobi.

LUQMAN: Unadharau wanawake wetu asilia sio? Labda tukukaribishe treni. Tunaenda Kigoma kuadhimisha miaka 10 ya Diamond Platnumz. Ikikupendeza na wewe unga mnyororo, upande treni. Hata Konde Boy na yeye anaalikwa, ingawa hajaalikwa, muhimu ajilipie tiketi ya kwenda na kurudi pamoja na malazi, chakula na manywaji. Kama ataenda na Sarah, amlipie tiketi. Hakatazwi mtu.

DK LEVY: Sisi tutakuwa Umakondeni tunajaza uwanja peke yetu bila kutegemea kiki wala madem. Mzungu wetu yuko bize na mimba. Huko Kigoma nendeni wenyewe maana tunajua nyie watu hata timu zenu za huko zinapenda sana ushindani badala ya mafanikio. Waulize Simba wa mbuga ya Msimbazi achana na yule Simba wa Mbuga ya Tandale.

LUQMAN: Hivi kitendo cha kuwafanya Ngassa, Kaseke na wachezaji wengine wa Yanga kuwa display ya kuuza hamira za vitumbua na maandazi ndio nini sasa? Mara Ngassa na jezi pamoja na viatu, analazwa kwenye godoro, kweli? Mtu huwa analala na viatu pamoja na mijezi ya njano kweli? Wakati wakifanywa display za godoro na hamira, Ngassa analalamika mitandaoni kuwa wazawa hawalipwi, wanaolipwa ni wageni. Halafu unasifu kuwa Yanga wapo vizuri. Eti wanamleta Uchebe. Unasajili wachezaji kutoka nje lakini wazawa waliopo hawalipwi. Kweli?

DK LEVY: Kwani kuna tofauti gani na kila kitu kuwa chini ya MO Simba? Kwani MO Simba ndo inayomiliki zile juisi na maji ya kunywa? MO Simba ndo wamiliki wa mashamba ya mkonge na kiwanda cha mafuta ya kupikia na sabuni? Kwani wachezaji wa Arsenal jezi ya Visit Rwanda wanaolipwa ni wachezaji au klabu? Acha chuki za kibwege bwege kama mtoto wa kambo.

LUQMAN: Na yule janki wa UD Songo ambaye Yanga walikuwa wanamtaka tayari kimeshaeleweka Msimambazi. Hivi Yanga wataambia nini mashabiki wao hiyo Januari 4? Anyways, kwa kukuongezea, Harmonize kama akimuomba msamaha Diamond na WCB, tiketi yake ya kwenda Kigoma atapewa, ili ajumuike na chama la WCB kusherehekea miaka 10 ya role model wake, Simba, Chibu Dangote.

DK LEVY: Simba kama umauti tu. Mauti yanamuondoa Kanumba yanaacha maiti na misukule ya filamu. Mauti yanamuondoa Nyerere yanaacha makapi na takataka za siasa. Mauti yanamuondoa Ngwair yanaziacha inzi za muziki. Ndo Simba inamuacha Okwi na Niyonzima wanakumbatia makaratasi uwanjani. Ndo maana wanamfukuza Uchebe bila sababu za msingi.

LUQMAN: Umeona mkwara wa Simba? Mechi ya kwanza baada ya Uchebe kuondoka, imeibugiza timu wiki kasoro siku moja, sita bila mwanawane. Ukiizingumzia Simba jitahidi kuwa mtu mwenye nidhamu. Sio unaongeaongea kama zile spika za mnada Karume sokoni, au za kwenye maduka ya simu Kariakoo.

DK LEVY: Unachofanya ni kuwasifia Al-Qaeda kulipua makaburi na kujisifia kuwa wameua. Ni kama wale waliolipua mochari na kujisifu wameua. Ndo wewe na wauza vijora wenzako wa Msimbazi kujisifu kuwafunga wale Machalii wa Arusha.

LUQMAN: Tufunge mjadala hapa, Harmonize tunakwenda naye Kigoma au haendi? Aseme mapema maana watu ni wengi, mabehewa yanakaribia kujaa. Zingatia yule ni role model wake.

DK LEVY: Konde Boy hawezi kwenda kwenye kilimo cha Mawese. Acha kufananisha Mawese na Korosho. Kifupi ni kwamba Harmonize ni mbunge wa Tandahimba yaani mwanasiasa. Na siasa zimepigwa marufuku mpaka 2020. Sasa unamualika Kigoma ili akakutane na wafuasi wa Zitto? Pambaneni na hali zenu muacheni Harmonize a.k.a Konde wa Tandahimba.
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad