Baraza la Wawakilishi la Marekani limepiga kura kuridhia kushtakiwa kwa Rais Donald Trump kwa kutumia vibaya madaraka yake na kuingilia uchunguzi wa Bunge.
Mchakato wa mwisho wa kura utalihusisha baraza la Seneti ambalo litakuwa na mamlaka ya kuamua kama anaweza kuondolewa madarakani au la
Matokeo ya mchakato huo ni kama ulikuwa ukijulikana mapema kutokana na baraza hilo kuwa na wingi wa wabunge wa chama cha Democratic.
Baada ya majadiliano ya masaa 10, wabunge walipigia kura vifungu viwili vya sheria; Shtaka la kwanza likiwa ni kutumia vibaya mamlaka aliyonayo lililotokana na madai ya kwamba Trump alijaribu kuishinikiza Ukraine kutangaza uchunguzi dhidi ya hasimu wake wa kisiasa na mgombea urais kupitia chama cha Democrats, Joe Biden.
Shtakala pili lilikua ni kuzuia shughuli za bunge la Kongresi kwasababu rais anadaiwa kukataa kutoa ushirikiano katika uchunguzi dhidi yake, kwa kukataa kutoa nyaraka za ushahidi na kuwazuwia wasaidizi wake kutoa ushahidi katika uchunguzi huo.
Kura katika kipengele cha kwanza cha uchunguzi, cha kutumia vibaya mamlaka zilikuwa 230 ndiyo na 197 hapana na kipengele cha pili cha kuzuia utendaji wa Kongresi zikawa 229 ndiyo na 198 hapana.
Baraza la wawakilishi lina nguvu ya kumshitaki rais kwa wingi mdogo wa kura, lakini baraza la Seneti litahitaji wingi wa theluthi mbili kumuondoa rais madarakani, hatua ambayo sio rahisi kufanyika kwa sababu Seneti inatawaliwa na wajumbe wengi kutoka chama cha Republican cha Rais Trump.
Rekodi zinaonesha kuwa hatua hiyo ni ya mara ya tatu kwa rais wa Marekani kushitakiwa.