Tume ya Madini yatangaza zabuni ununuzi wa maeneo yenye leseni hodhi za madini



Na Greyson Mwase, Dodoma
Tume ya Madini  imetangaza zabuni kwa ajili ya ununuzi wa maeneo  10 yenye leseni hodhi za madini na yenye ukubwa wa kilomita za mraba 381.89 yaliyopo katika maeneo ya Ngara – Kagera, Kahama- Shinyanga, Chunya- Mbeya, Bariadi na Busega – Simiyu, Morogoro, Nachingwea – Lindi ambayo awali leseni hodhi zake zilikuwa zimerudishwa Serikalini.

Uamuzi huo umetangazwa leo tarehe 19 Desemba, 2019 na Mwenyekiti wa Tume ya Madini, Profesa Idris Kikula kupitia mkutano wake na waandishi wa habari  uliofanyika jijini Dodoma na kuhudhuriwa na Kamishna wa Tume ya Madini, Dkt. Athanas Macheyeki, Katibu Mtendaji wa Tume ya Madini, Profesa Shukrani Manya pamoja na watendaji wengine wa Tume ya Madini.

Profesa Kilula alifafanua kuwa, awali mwaka 2017 Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania lilipitisha marekebisho ya Sheria ya Madini Sura Namba 123 na kanuni zake ambapo  pamoja na mambo mengine, zilizokuwa leseni hodhi za madini ( retention licence) zilirudishwa Serikalini .

Alisema baada ya marekebisho hayo maeneo yote 10  yenye ukubwa wa kilomita za mraba 381.89 yalirudishwa Serikalini na kuongeza kuwa, wachimbaji wa madini wengi wamekuwa wakiulizia maeneo hayo mara kwa mara lengo likiwa ni kuomba leseni za uchimbaji madini.

Aliendelea kusema kuwa, baada ya uchambuzi wa kina kufanyika, Serikali kupitia  Tume ya Madini, maeneo yote 10 yaliyokuwa na leseni hodhi yatatolewa kwa zabuni na kukaribisha kampuni za uchimbaji wa madini na watu binafsi  wenye uwezo wa fedha na utaalam katika miradi ya uchimbaji wa madini na wenye nia ya kuendeleza miradi ya madini ya nickel, dhahabu na rare earth elements kuomba zabuni hizo.

Aliongeza kuwa, mwekezaji atakayeonesha nia ya kuwekeza katika maeneo hayo atakuwa na jukumu  la kufanya kazi na kuwaendeleza wachimbaji wadogo wa madini.

Wakati huo huo, Katibu Mtendaji wa Tume ya Madini, Profesa Shukrani Manya akielezea hatua zinazochukuliwa kwa wamiliki wa leseni  wasioendeleza maeneo yao, aliwataka wamiliki na waombaji wote wa leseni za utafutaji na uchimbaji wa madini wenye mapungufu kurekebisha mapungufu  hayo ndani ya siku 30 kuanzia sasa.

Alifafanua mapungufu hayo kuwa ni pamoja na leseni ambazo hazifanyiwi kazi, leseni ambazo hazijalipiwa ada ya pango la mwaka, maombi ambayo hayajalipiwa ada ya maombi na maombi yaliyokosa viambatisho muhimu kwa mujibu wa sheria.

Profesa Manya alitaja mapungufu mengine kuwa ni pamoja na waombaji waliokidhi vigezo vya kupewa leseni lakini hawajalipa ada ya maandalizi na wamiliki ambao leseni zao zimeshatolewa lakini hazijachukuliwa.

Alifafanua kuwa mpaka sasa leseni zaidi ya 134 za utafutaji na uchimbaji wa kati wa madini hazijachukuliwa na zaidi ya maombi 450 ya leseni za utafutaji yana mapungufu.

Akielezea hatua zitakazochukuliwa kwa kampuni au watu binafsi walioaminiwa na Serikali na kupewa leseni lakini wameshindwa kutekeleza masharti ya leseni kwa mujibu wa Sheria ya Madini,  alisema leseni ambazo hazijalipiwa ada ya pango kwa mwaka, leseni ambazo hazifanyiwi kazi na leseni ambazo zimekwishatolewa lakini hazijachukuliwa zitaandikiwa hati ya makosa na yasiporekebishwa zitafutwa kwa mujibu wa sheria.

Aidha alisema kuwa, maombi yote ya leseni za utafutaji na uchimbaji wa kati yenye mapungufu yataondolewa kwenye mfumo wa utoaji wa leseni ili waombaji wengine wenye sifa pamoja na wachimbaji wadogo waweze kuomba maeneo hayo.

Aliendelea kusema kuwa, maombi ambayo yamekidhi vigezo vya kupewa leseni lakini hayajalipiwa ada ya kuandalia leseni yataondolewa kwenye mfumo ili waombaji wengine wenye sifa waweze kuomba maeneo hayo.

Alisisitiza kuwa tangazo la zabuni husika linapatikana katika tovuti ya Wizara ya Madini ambayo ni (www.madini.go.tz)  Tume ya Madini (www.tumemadini.go.tz) magazeti ya Habari Leo na Daily News ya tarehe 20 Desemba, 2019 pamoja na blogs na mitandao ya kijamii.

Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad