Ujerumani imeishutumu Marekani kwa kuingilia masuala yake ya ndani katika matamshi ya hasira kuhusiana na uamuzi wa Marekani kuweka vikwazo dhidi ya makampuni yanayohusika na mradi wa kusambaza gesi ya Urusi
Urusi na Umoja wa Ulaya pia zimetoa taarifa zinazokosoa vikwazo hivyo, siku moja baada ya rais wa Marekani Donald Trump kutia saini kuwa sheria hatua ya kuzuia mali na upatikanaji wa visa kwa wale wanaohusika katika mradi huo wa Nord Stream 2.
Wabunge wa Marekani wanataka kuzuia kile wanachokiona kuwa ni ongezeko la utegemezi wa nishati kutoka Urusi katika mataifa ya Ulaya magharibi kwa kulenga mradi huo, ambao una lengo la kuongeza maradufu usambazaji wa gesi asilia kutoka Urusi nchini Ujerumani kupitia katika bomba lililowekwa chini ya bahari ya Baltiki.
Vikwazo hivyo vinalenga wakandarasi wanaofanyakazi katika kutandika bomba hilo la Nord Stream 2, mradi wenye thamani ya euro bilioni 10 unaotarajiwa kukamilika mapema mwaka 2020, na mradi mwingine wa gesi wa Urusi , unaojulikana kama TurkStream.
Licha ya kuwa bunge la Marekani waliunga mkono kwa kiasi kikubwa vikwazo, kulikuwa na baadhi wamekosoa hatua hiyo ambayo kimsingi inawaadhibu washirika wa NATO kama Ujerumani.
Wakati msemaji wa Umoja wa Ulaya amekosoa kile alichokiita "uwekaji wa vikwazo dhidi ya makampuni ya Umoja wa Ulaya yanayofanyakazi halali", serikali ya Ujerumani imesema Berlin inakataa "aina hii ya vikwazo dhidi ya mataifa ya kanda".
"Hatua hii itayaathiri makampuni ya Ujerumani na Umoja wa Ulaya na kufikia katika uingiliaji wa masuala yetu ya ndani," amesema msemaji wa kansela Angela Merkel , Ulrike Demmer.
Msemaji wa wizara ya mambo ya kigeni ya Urusi Maria Zakharova ameishutumu Marekani kwa kuendeleza nadharia ambazo zinazuia biashara ya dunia, na kuongeza katika ukurasa wake wa Facebook: "Hivi karibuni watadai kuwa tuache kupumua."