Vijana bila kuchapa kazi vyuma vitabana kweli kweli - Katibu Mkuu CCM



Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Dkt. Bashiru Ally amewaleza vijana umuhimu wa kuwa na maarifa kwani ukiwa na shahada pekee sio pesa, ila maarifa yako ndio hutengeneza pesa, hivyo vijana ni lazima wawe wabunifu, bila kuchapa kazi maisha yataendelea kubana.

Dkt. Bashiru amesema, yeye ni Katibu Mkuu wa CCM kwa sasa, lakini hakuna magulio asiyoyafahamu wilayani Bukoba, kwa kuwa alipokuwa anasoma na baada ya kuhitimu masomo yake, kazi kubwa aliyokuwa akiifanya bila uwoga ni uchuuzi kwenye magulio kazi ambazo vijana wengi wakiwa na shahada kichwani hawawezi kuzifanya.

Dkt. Bashiru ameyasema hayo, Desemba 29, 2019 alipokuwa akitoa salamu za Chama wilayani Muleba kata ya Mayondwe katika shughuli ya dua iliyojumuisha maombi mbalimbali pamoja na kuiombea amani nchi yetu.

“Vijana bila kuchapa kazi maisha yatabana, na vyuma vitabana kwelikweli, mimi ni Katibu Mkuu kwa sasa hakuna magulio nisiyoyafahamu hapa Bukoba na Muleba kwa kiasi, wakati nasoma na baada ya kuhitimu masomo kazi kubwa niliyoifanya kwa muda mrefu ni uchuuzi kwenye magulio kazi ambayo vijana wengi wakiwa na shahada kichwani hawapendi kuzifanya.’’ Bashiru ameeleza

Ameongeza kuwa, ukiwa na elimu ya shahada kichwani hiyo sio pesa, ila maarifa yako ndio yatatengeneza pesa akimtolea mfano Bw. Jafari Swalehe waliosoma naye darasa moja shule ya msingi Katerero na kuishia darasa la saba mkazi wa Bukoba vijijini ambaye kwa sasa ni mkulima mkubwa wa mbogamboga na matunda wilayani hapo.

Wakati huo huo, Dkt. Bashiru ameeleza wazi kuwa, CCM inajukumu la kutunga Sera wezeshi ili kundi kubwa la vijana waweze kupata mazingira mazuri ya fursa mbalimbali zikiwemo biashara, kilimo na viwanda, ambalo wameendelea kulifanya na katika Sera na Ilani ijayo suala hili litapewa uzito wa pekee ili kuwezesha kundi kubwa la vijana kupata na kumudu fursa za kimaendeleo.

Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad