Vita ya Meya Chadema, madiwani CCM yafikia patamu


Dar es Salaam. Unaweza kusema vita ya Meya wa Jiji la Dar es Salaam, Isaya Mwita na madiwani wa CCM waliowasilisha ombi la kutokuwa na imani naye kwa madai ya kuwa anatumia vibaya ofisi imefikia patamu.

Tayari timu ya kumchunguza Meya huyo ambaye ni diwani wa Kigamboni (Chadema) imeshaundwa na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda na imewahoji madiwani kadhaa.

Taarifa zilizolifikia Mwananchi zimeeleza jinsi Mwita alivyojibu tuhuma hizo, zikisisitiza kuwa kwa majibu yake huenda hoja iliyotolewa ikakosa nguvu.

Meya wa Temeke, Abdallah Chaurembo alikiri wajumbe wa CCM kusaini ombi la kutokuwa na imani na Mwita kutokana na tuhuma anazokabiliwa na kuahidi kutoa ufafanuzi wa kina kesho.

Barua walizoandikiwa madiwani walioitwa kuhojiwa na timu hiyo ambayo Mwananchi imeiona, inaeleza kuwa inafanya kazi ya kupitia nyaraka mbalimbali zinazomhusu Mwita. “Nimeombwa nikutaarifu kuwa unatakiwa kukutana na timu ya uchunguzi Jumanne Desemba 17, mwaka huu au Jumatano kuanzia saa 3 asubuhi,” inaeleza barua aliyoandikiwa mmoja wa madiwani, ikifafanua kuwa timu hiyo inafanya kazi zake katika ofisi ya mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam. Barua hiyo iliyoandikwa na mkurugenzi wa Jiji la Dar es Salaam, Spora Liana inaeleza kuwa malalamiko dhidi ya Mwita yametolewa na madiwani wa CCM.

Mwita anadaiwa kutotumia Sh5.8 bilioni za Shirika la Usafiri Dar es Salaam (Uda). Fedha hizo ni asilimia 51 ya hisa zilizotolewa na Kampuni ya Simon Group kama sehemu ya ununuzi wa asilimia 51 ya hisa za Uda. Tuhuma nyingine ni kutumia vibaya gari ya ofisi ambayo alipata nalo ajali, kushindwa kuongoza kikao cha baraza la madiwani na kusababisha Meya wa Ubungo, Boniface Jacob kugombana na Meya wa Temeke, Abdallah Chaurembo na kudaiwa kuwapendelea baadhi ya mameya kuingia kwenye kamati za fedha.


Mwita ameshajibu tuhuma hizo baada ya kupewa siku tano na ofisi ya mkurugenzi jiji la Dar es Salaam. Amelieleza Mwananchi jana kuwa amepewa barua yenye tuhuma zake Mei 6, mwaka huu licha ya kutotaka kuziweka hadharani kwa madai ya kuwa ameshazijibu na anasubiri hatua nyingine, “nimeshapokea barua tayari na tuhuma nimeshazijibu.”

Chanzo kimelieleza Mwananchi kuwa Meya huyo alijibu kuwa hahusiki na kukwamisha matumizi ya Sh5.8 bilioni kwa kuwa fedha hizo zinaidhinishwa na kamati ya fedha. “Kuhusu tuhuma za gari anadai haimhusu kwa sababu yeye si dereva. Alizungumzia kuhusu ajali ya gari akidai hakuwepo bali dereva aliliegesha sehemu na kwenda kula likagongwa. Pia suala la Jacob na Chaurembo kufanya vurugu, hilo amesema halimhusu maana walikuwa wakigombea kura katika uchaguzi,” kilieleza chanzo hicho.

Tayari baadhi wajumbe wa CCM wameitwa na ofisi ya mkurugenzi wa jiji kuhusu suala hilo, huku wanaotoka Chadema wakiwa kikwazo kutokana na kutofika katika tume hiyo kuhojiwa.

Kwa upande wake, Jacob amekiri kupokea barua ya wito, lakini hajaenda huku akibainisha kuwa mchakato huo umelenga kumuondoa Mwita kwa sababu za kisiasa, jambo ambalo si zuri kwa mazingira ya sasa.

“Haya mambo ya kisiasa binafsi sijui kosa la Mwita kwa sababu sijaenda kwenye hicho kikao chao nilikuwa na masuala ya uchaguzi wa ndani ya chama. Kwa muda mrefu wamekuwa wakimtafuta Mwita sasa hii ni sababu yao ya kumuondoa,” alisema Jacob.

Mjumbe mwingine wa baraza hilo wa Chadema, Patrick Assenga amekiri kupokea barua ya wito wa mahojiano kuhusu utendaji kazi wa Mwita lakini hajaenda kwa kuwa alikuwa na kazi nyingi.

“Nikipata muda nitakwenda kuwaeleza ukweli, hizi tuhuma ni za kubumba na wanayoyafanya si sawa. Wengine ni marafiki tunawauliza kwa nini mnafanya hivyo wanatuambia ni maelekezo,” alisema Asenga.
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad