Na Paschal Malulu-Kahama.
Wananchi wilayani Kahama mkoani Shinyanga wametakiwa kuacha kufunga biashara kinyemela bila kutoa taarifa katika mamlaka za mapato Tanzania (TRA) ili kujiepusha na usumbufu unaoweza kujitokeza pindi akihitaji kuanzisha biashara nyingine.
Hayo yamebainishwa katika semina ya mlipa kodi kwa waandishi wa habari wilayani Kahama na afisa elimu kwa mlipa kodi na huduma mkoa wa Shinyanga Antony Faustine amesema wananchi wamekuwa wakiacha kimya kimya biashara bila taarifa za kufunga biashara.
Amesema mfanyabiashara anapofunga biashara kutokana na kuyumba kiuchumi anatakiwa kuwasiliana na TRA ya eneo husika ili kusitisha biashara kwa kuandika barua itakayowekwa kwenye kumbukumbu zake ambayo akihitaji kuanzisha biashara kwa mara nyingine ataendelea kutumia TIN namba yake ile ya awali.
Faustine amesema kuna baadhi ya wafanyabiashara wanafunga biashara lakini wanapohitaji kuanzisha tena wanatumia majina ya watu wengine kitu ambacho kinaweza kusababisha kuibiwa mali zake hivyo wanatakiwa kutoa taarifa kwani mamlaka ya mapato haimzuii mtu yeyote kufunga biashara.
Kwa upande wake kaimu meneja wa mamlaka ya mapato mkoa wa Kahama Wilson Mashauri amesema pia wananchi wanatakiwa kutii mamlaka ili kujiepusha na makosa yasiyo ya lazima kwani kufunga biashara kimyakimya inaweza kusababisha kuwa na deni la kodi kubwa kwani siku akihitaji kufungua tena deni atalikuta.
Amesema mfumo wa TRA una uwezo wa kubaini mteja au mfanyabiashara ambaye alishawahi kufungua biashara kwani katika usajili mfumo wa alama za vidole kwa mfanyabiashara hutumiwa hivyo taarifa zake zitaonekana pindi atakapokuwa anataka kufungua na kupata namba (TIN) mpya ya biashara.
Mshauri ameongeza kuwa wafanyabiashara na wananchi kwa ujumla wanatakiwa kuendelea kutumia mashine za EFD ili serikali iweze kukusanya mapato ambayo yatasaidia katika miradi mbalimbali lakini pia kukwepa kutumia mashine za EFD ni ukiukwaji wa sheria hivyo ambaye akibainika sheria itafuata mkondo wake.
Amesema mwananchi anao wajibu wa kutoa taarifa za mfanyabiashara yoyote ambaye ametoa huduma na hukutoa listi kwani kukaa kimya kwa mwananchi aliehudumiwa wote wanakuwa wana makosa ambapo kila mmoja taadhibiwa kwa mujibu wa sheria.
Aidha mafunzo ya elimu ya mlipa kodi kwa wandishi wa habari wilayani Kahama mkoani Shinyanga yamefanyika jana Disemba 27, 2019 katika ukumbi wa mamlaka ya mapato nchini TRA wilayani humo.