Wafanyabiashara Watekwa na Al-shabaab
0
December 28, 2019
- Wafanyibiashara wawili walikuwa wakisafirisha miraa kuenda Garissa walipotekwa nyara
- Wazee kutoka eneo la Liboi walisema magari mawili ya wafanyibiashara hao yalionekana yakielekezwa kwenye mpaka wa Somali
- Kisa hicho kinajiri wakati ambapo serikali bado inafanya mazungumzo na kundi hilo ili madaktari wa Cuba waliotekwa nyara waachiliwe
Polisi mjini Garissa wameanzisha juhudi za kuwaokoa Wakenya wawili wanaoaminika kutekwa nyara na wanachama wa kundi la al-shabaab.
Inaarifiwa wawili hao, Abdulahi Isaack Harun na Abdi Hassan Ilkaase walitekwa nyara Alhamisi, Disemba 26, saa moja asubuhi.
Garissa: Wauza miraa watekwa nyara na al-shabaab
Watu wawili waliokuwa wakisafirisha miraa Garissa walitekwa nyara na watu wanaoshukiwa kuwa wa kundi la al-shabaab.
Polisi walisema wawili hao walikuwa wakipeleka miraa hiyo Liboi, lakini kufika Wardeglo Dam wakatekwa nyara na inashukiwa walipelekwa Somalia.
"Iliripotiwa na wazee wa Liboi kuwa magari mawili yaliyokuwa yakisafirisha miraa kuenda Liboi yalitekwa katika eneo la Wardeglo yakiwa na watu wawili," polisi walisema.
"Magari hayo yalionekana mara ya mwisho eneo la Osman Baret kwenye mpaka wa Abdisugow na Gubahadhe mpakani Somalia 8.30am," polisi walisema.
Garissa: Wauza miraa watekwa nyara na al-shabaab
Polisi walisema magari mawili yaliyokuwa na miraa yalielekezwa Somalia.
Hayo yanajiri wiki mbili tu baada ya al-shabaab kuteka nyara basi moja kutoka Garissa na kuwaua watu kumi wakiwemo maafisa wa polisi sita.
Vile vile, serikali imekuwa katika juhudi za mazungumzo na kundi hilo baada ya madaktari wa Cuba waliokuwa wametumwa Mandera kutekwa nyara.
Kundi hilo limekuwa likidai kima cha shilingi milioni 150.
Source: Tuko
Tags