Serikali ya wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (Daruso) nchini Tanzania imetoa saa 72 kwa Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) kutoa mikopo kwa wanafunzi waliokosa, vinginevyo wanafunzi watakutana nje ya ofisi za bodi hiyo zilizopo Mwenge Dar es Salaam Desemba 19, 2019.
Taarifa iliyotolewa jana na Waziri wa Habari na Mawasiliano wa Daruso, Judith Mariki ilisema wamefikia uamuzi huo baada ya changamoto ya kukosekana kwa mikopo kwa wanafunzi wengi wa mwaka wa kwanza tangu chuo kifunguliwe huku baadhi ya wanafunzi wanaoendelea wakikatwa fedha zao.
Mariki alisema baada ya juhudi kubwa ya kufuatilia na mazungumzo kugonga mwamba, serikali imefanya mazungumzo ya ndani kwa ndani iliyojumuisha mihimili mitatu ya serikali hiyo.
“Daruso inatoa saa 72 kwa HESLB iwe imeleta allocations za mikopo ya wanafunzi waliokaa chuo tangu chuo kifunguliwe bila fedha, ilihali ni mkataba halali kabisa na hakuna sababu za wao kutaabika hivi,” ilisema taarifa ya Daruso.
Daruso pia imeitaka HESLB kurejesha makato ya fedha za vitabu, mafunzo kwa vitendo na utafiti.
“Iwe imewapa mikopo ya wanafunzi wa mwaka wa kwanza ambao rufaa zao zimetupiliwa mbali ilihali wao ni wahitaji,” ilisema Daruso huku ikitaka ofisa mikopo aliyepo chuo hapo (wanamtaja) kubadilishwa.