WCB Kusafiri na Treni ya Deluxe Kuelekea Kigoma


Kampuni ya Wasafi (WCB) ambayo pia inasimamia wanamuziki wa  kizazi kipya na vyombo vya habari nchini  inatarajia kufanya safari kutoka Dar es Salaam kuelekea Kigoma kwa kutumia treni ya kisasa ya Deluxe katika tamasha la kuadhimisha miaka 10 ya Mkurugenzi  wa kampuni ya Wasafi na mwanamuziki maarufu nchini Diamond Platnum Desemba 28, 2019.



Lengo la kufanya safari na treni ya Deluxe kuelekea Kigoma ni kuunga mkono jitihada za Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania chini ya Mhe. Rais Dkt. John Pombe Magufuli za kuboresha miundombinu ya sekta yaa reli nchini, pia kuwahamasisha wananchi kutumia usafiri wa treni kwani ni usafiri wa uhakika, salama na wa gharama nafuu.

‘’Serikali ya awamu ya tano imefanya mambo mengi katika sekta ya usafiri na sio vibaya kuunga jitihada za Mhe. Rais kwasababu nchi za wenzetu usafiri wao mkubwa ni treni hivyo treni za mwendokasi zitaleta mapinduzi katika sekta ya usafiri wa treni” alisema Diamond

Mkurugenzi wa wasafi pamoja na viongozi wa kundi la WCB walifika katika ofisi ya TRC makao makuu jijini Dar es Salaam Desemba 13, 2019, ambapo walifanya mazungumzo na Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Reli Tanzania na baadhi ya Viongozi wa Shirika kuhusu safari hiyo ya kihistoria itakayohusisha wasanii wa WCB pamoja na mashabiki zaidi ya 200 wa kampuni hiyo watakaojumuika katika safari hiyo.

Aidha Nasib amesema kuwa treni ni usafiri wa uhakika na hauna wasiwasi, pia kwa jiji la Kigoma treni ndio usafiri pekee unaotumika zaidi kusafirisha abiria na mizigo kutoka na kuelekea mikoa mingine, ameongeza kuwa raha ya kwenda Kigoma ni kwenda kwa kutumia usafiri wa treni.
 “Ukizungumza kigoma unazungumzia treni, raha ya kufika kigoma ni kwenda kwa kutumia treni pia huu ni usafiri wa uhakika na hauna wasiwasi tofauti na usafiri mwingine hivyo nampongeza Mhe. Rais wa Jamhuri wa Muungano wa Tanzania kwa mapinduzi anayoyafanya” alisema Diamond Platinum

Halikadhalika Msanii Diamond Platinum amemshukuru Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Reli Tanzania Ndugu Masanja Kungu Kadogosa kwa nafasi aliyowapatia ya kusafiri na treni ya Deluxe, kwa sababu amekuwa akiunga mkono shughuli za wasnii mara kadhaa. Diamond ametoa rai kwa wananchi na kuwaambia kuwa treni ni usafiri mzuri, wa uhakika  na ni salama hivyo watumie usafiri huo.
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad