Yanga Hamna KITU Yabanwa Mbavu na Vibonde
0
December 25, 2019
YANGA imeshindwa kutamba mbele ya vibonde Mbeya City ambao wanashika nafasi ya 18 kwenye msimamo wa Ligi Kuu Bara baada ya kukubali suluhu Uwanja wa Sokoine jijini Mbeya.
Yanga wamebaki nafasi yao ile ile ya tisa ingawa imeongeza pointi moja na kufikisha pointi 18 huku wakiwa wamecheza mechi tisa mpaka sasa, wameshinda mitano, wametoka sare mechi tatu wamepoteza mechi moja.
Ilikuwa ngumu kwa wachezaji kutulia na mipira miguu kutokana na uwanja huo kutuwama maji na kufanya wawe wanabutuabutua mipira huku ufundi ukikosekana.
Wachezaji walionekana kuwa na wakati mgumu wa kucheza soka la maana katika kusaka mabao kwa dakika 45 za kipindi cha kwanza, huku wachezaji wakipiga mipira mirefu iliokuwa inakutana na vikwazo vya mabeki.
Ukiachana na timu hizo kushindwa kuonyesha ufundi kutokana na wachezaji kuteleza kwa hali ya uwanja ilivyokuwa pia wachezaji walikuwa wakitumia nguvu katika kutafuta mpira.
Wachezaji wa Mbeya City walionekana kutumia mabavu na kusababisha faulo zilizokuwa zikiwasaidia Yanga ambao walikuwa wakimtumia, Patrick Sibomana. Hata hivyo faulo hazikuweza kuzaa matunda kutokana na mipira mingi kuangukia vichwani vya mabeki wa Mbeya City na mikononi mwa mlinda mlango.
Hata hivyo straika wa Yanga, David Molinga alionekana kupambana na kutumia mwili wake vyema kuhakikisha anapenya ngome ya mabeki wa Mbeya City, lakini alijikuta akishindwa kutimiza lengo.
Licha ya Molinga kupata nafasi ya kuitoka ngome ya Mbeya City kila mara na kuingia ndani ya 18, hata hivyo juhudi zake hazikuwa na faida.
Dakika ya 58 Molinga alipiga shuti kali na kama si uimara wa kipa wa Mbeya City kupangua shuti basi ingekuwa muda wa mashabiki wa Yanga kucheka.
Kipindi cha pili mchezo ulianza kwa kasi huku kila timu ikicheza kwa tahadhari kutokana na hali ya uwanja, na dakika ya 72, Peter Mapunda alikosa nafasi ya wazi baada ya shuti lake kutoka nje.
Mwanaspoti
Tags