Zitto, Mtaka wanavyochuana kusoma vitabu


Moshi. Wakati mwamko wa Watanzania kujisomea vitabu ili kuongeza maarifa ukiwa chini, kuna watu wa kada tofauti wakiwamo viongozi wa kisiasa wanachuana kwa kusoma vitabu vingi huku wengine wakijisomea hadi vitabu 40 kwa mwaka.

Hata hivyo, wakili wa kujitegemea wa jijini Dar es Salaam, Frank Mushi anaweza kuongoza kwa usomaji ambapo licha ya kuwa ni mtunzi wa vitabu, lakini husoma vitabu hadi 300 kwa mwaka.

Mbunge wa Kigoma Mjini na Kiongozi Mkuu wa ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe, Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Antony Mtaka na Mhariri Mtendaji Mkuu wa Mwananchi Communications Limited (MCL), Bakari Machumu wameiambia Mwananchi kuwa wamebobea katika kusoma vitabu.

Mwaka 2017, Zitto anasema alisoma vitabu 39, mwaka 2018 vitabu 49 na mwaka huu 2019 vitabu 34 wakati 2017, Mtaka alisoma vitabu 20, mwaka 2018 alisoma vitabu 17 na mwaka huu wa 2019 amesoma vitabu 23.

Wakili Mushi ametunga vitabu 60 na viko katika hatua mbalimbali za umaliziaji huku vitatu vikiwa tayari vimeshachapwa.

Ameliambia Mwananchi kuwa Watanzania wengi hawana utamaduni wa kusoma vitabu.

“`Habit’ (tabia) ya kusoma vitabu si jambo ambalo mtu anazaliwa nalo. Ni hulka ambayo anaweza kujifunza kupitia kwa wazazi au shuleni. Mimi nasoma vitabu kati ya 250 na 300 kwa mwaka.

“Shule nyingi hazifundishi kusoma vitabu bali zinafundisha kusoma `summary’ (muhtasari). Unaweza kukuta mtu anafahamu `summary’ ya kitabu cha Chinua Achebe lakini hajakisoma.

“Wengi wetu tuna uvivu wa kuchambua. Ukisoma kitabu lazima uchambue kujua mtunzi alikusudia nini na nini amekisema na kipi hakukisema,” alisema Mushi.

Wakili huyo amependekeza kuanzishwa klabu shuleni kwa ajili ya kusoma vitabu ili kujenga hamasa ya watu kusoma, lakini akasema lipo tatizo la uwapo wa vitabu vya kusomwa na rika zote.

Akizungumzia tabia yake ya kusoma vitabu, Zitto alisema idadi ya vitabu alivyosoma kwa mwaka 2019 imepungua kutokana na shughuli zake kuongezeka ikiwamo ujenzi wa chama chake na kesi alizonazo mahakamani.

“Mwaka 2019 ndiyo nimekanyaga mahakamani mara nyingi zaidi kuliko wakati wowote wa maisha yangu. Majukumu yanapozidi, muda wa kujisomea unapungua,” alisema Zitto.

Hata hivyo, anasema bado amejitahidi kusoma vitabu kadhaa na amesema; “Ingizo jipya ni riwaya za mwandishi wa kituruki, Orhan Pamuk ambaye nimesoma vitabu vyake vinne mwaka huu. Amenifanya kupenda kusoma kazi za waandishi wengine kutoka Uturuki.”

“Hii ni kutokana na riwaya zake zenye mchanyato wa masuala ya siasa za Uturuki, utamaduni, mapenzi na maisha ya watu kiujumla. ‘A Strangeness in Mind’ ndiyo ilinivutia kuliko zote.

“Ni riwaya inayoeleza maisha ya kijana Mevlut aliyetoka shamba na kuhamia mjini na namna maisha yake yalivyobadilika kwa kasi. Inaonyesha tamaduni za Kituruki kuhusu ndoa na mahusiano.

“Kitabu hiki ukikisoma kitakufanya uione Uturuki na mapinduzi ya kijeshi yalivyoigubika mwaka hadi mwaka, pamoja na mtanziko wa siasa zenye kuheshimu misingi ya dini au kufuata umagharibi.”

“Nilisoma pia riwaya nyingine zikiwemo kazi za watunzi mliozoea kuwaona kama Jefrey Archer na John Grisham katika orodha zangu za miaka ya hivi karibuni,”anasema Zitto na kuongeza;-

“Pia nilimsoma Mzee Makaidi, kazi yake aliyoandika miaka mingi nyuma. Mwaka huu nimevutiwa sana na kazi za mtunzi wa kitanzania anayechipukia Bwana Lello Mmasy.

“Riwaya ya Mimi na Rais ilinikosesha usingizi kwani sikutamani kuacha kuisoma. Ni riwaya iliyosadifiwa vizuri na kwa ubunifu mkubwa huku ikichora picha halisi yenye kuvutia msomaji.

“Riwaya hii naifananisha na ile ya A Man of The People ya Chinua Achebe kwa ubunifu na labda utabiri. Nchi ya Stanza na Rais wake Bwana Costa aliyekuwa anaharibu uchumi wa Taifa lake,” alieleza.

Zitto alisema mwaka huu amebahatika kupata vitabu vya baadhi ya viongozi wa zamani kikiwamo cha Rais wa Awamu ya Tatu Mzee Benjamin Mkapa ambacho amekitoa mwaka huu cha `My Life, My Purpose (Maisha yangu, Kusudio Langu).

“Kabla ya hapo, Mzee Njelu Kasaka aliyekuwa mbunge na Katibu wa Kundi la G55 lililotaka Serikali ya Tanganyika alitoa kitabu chake pia. Vitabu hivi ni muhimu sana katika kuifahamu Tanzania,” aliongeza.

Zitto alisema amesoma pia kitabu cha Balozi Wilibrod Slaa kinachoeleza maisha yake na pia nini kilitokea katika chama cha Chadema mwaka 2015.

“Si kitabu cha kupuuza kwani kina mafunzo mengi kwa wanasiasa. Nasikitika Balozi Slaa kuna vitu hakuandika labda kupitia kwake ningeweza kujua haswa ushiriki wake katika kufukuzwa kwangu kwenye chama ambacho yeye alikuwa Katibu Mkuu,” alisema.

Zitto alisema mwaka huu kitabu kilichomvutia zaidi kuliko vyote kinaitwa `Two Weeks in November’ kilichoandikwa na Douglas Rogers.”

Zitto anasema kitabu hicho kinaeleza namna watu mbalimbali waliokuwa maadui na marafiki, hadi kufikia kuviziana kuuana, walivyoungana na kushirikiana kumwondoa madarakani Rais Robert Mugabe wa Zimbabwe.

Alisema licha ya kwamba kuondolewa kwa Mugabe madarakani hakujaleta ahueni kwa wananchi wa Zimbabwe ingawa anaongeza mbinu, mikakati na mafunzo ndani ya kitabu hicho ni somo kwa wapigania demokrasia.

“Kila Rais Afrika, kila Mkuu wa Majeshi, kila Kiongozi wa Upinzani na kila mwanasiasa mwenye kujitambua asome kitabu hiki. Akifanye rejea yake ya mara kwa mara,” anasema Zitto.

Mtaka alisema katika vitabu vyote alivyosoma, kilichomvutia zaidi ni cha`Making Africa Work, a Handbook for Economic Succes’.

“Nimekisoma kitabu hiki kina mengi ya kutufunza waafrika na hasa viongozi. Kiujumla kimeangazia urasimu wa watunga sera na watenda maamuzi wa kiafrika,” alisema Mtaka na kuongeza;-

“Kinaelezea namna wanavyojichelewesha kwenye dunia ya ushindani. Kimetahadharisha pia ongezeko kubwa la watu barani Afrika hasa vijana na changamoto ya ajira.”

Mtaka alisema kitabu hicho kimesheheni uzoefu wa serikali za Afrika kikielezea tulipotoka, tulipo na namna ya kufika tunakotaka kwenda akisisitiza kuwa si kitabu cha mtu kukosa kukisoma.

“Kwa mtu anayependa matokeo katika uchumi, uongozi na maendeleo ya jamii yake si kitabu cha kukosa. Ndio maana Rais wa zamani wa Malawi, Joyce Banda alisema alitamani angekipata kabla hajawa Rais,” alisema Mtaka.

Mhariri Mtendaji Mkuu wa Kampuni Mwananchi Communications Limited (MCL), Bakari Machumu alisema amesoma vitabu zaidi ya 50 kwa njia ya sauti kupitia programu ya ‘Blibnkist’ aliyoiweka kwenye simu yake ya mkononi anayoilipia kwa mwezi au mwaka kutokana na uhitaji.
“Kupitia programu hii, kitabu kimoja unakisikiliza kwa dakika 15 hadi 20, unaweza kusikiliza ukiwa katikati ya watu, barabarani hasa kwenye foleni, badala ya kusikiliza redio mimi nasikiliza kitabu na ndiyo maana nimesoma idadi hii,” alieleza Machumu.
Alisema mwisho wa kila kitabu kunakuwa na muhtasari unaoeleza mafunzo yanayotokana na kitabu husika.
Alipoulizwa kitabu alichofurahia zaidi, Machumu alijibu kinaitwa ‘The Dichotomy of Leadership’ kilichoandikwa na ‘Jacko Willink na Leif Babin’ ambao ni wanajeshi wa kimarekani, na kilichomfurahisha wanavyoelezea jinsi ya kushinda vita ya baharini, nchi kavu na angani.
Alisema mbinu hiyo ya kushinda vita, inafaa hata kwenye biashara.

“Unajua biashara ni vita, kitabu hiki kinaeleza vizuri mbinu za kutumia lakini jambo muhimu ni kuhakikisha shughuli unayofanya hata kama ni ya kuajiriwa lazima ujimilikishe mwenyewe,” alisema Machumu.

Machumu aliongeza kitabu hicho kinafundisha jinsi ukiwa kiongozi sehemu yoyote unavyopaswa kuwaamini watu walio chini yako na kuwaacha wakafanya kazi na uamuzi pasipo kuwaingilia ili kujenga viongozi wa baadaye na wakati mwingine mtu akikosea kazini si lazima kutoa adhabu.
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad