Sakata la UMEYA Dar es Salaam...Kura Moja Yashikilia Umeya wa Chadema
0
January 28, 2020
By Bakari Kiango na Tausi Ally, Mwananchi
Dar es Salaam. Wakati hali ikiwa bado haijatulia, imebainika kuwa kura moja ya mjumbe wa baraza la madiwani wa Jiji la Dar es Salaam ndio imeshikilia umeya wa Isaya Mwita.
Kuna mvutano mkali wa suala la umeya wa Jiji la Dar es Salaam kati ya CCM kwa upande mmoja dhidi ya Chadema.
Madiwani wa Jiji la Dar es Salaam walikutana juzi huku wale wa CCM wakiitisha kura ya kutokuwa na imani dhidi ya Meya Mwita anayetokea Chadema kufuatia ripoti ya kamati iliyoundwa na mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda kuchunguza tuhuma dhidi ya meya huyo ya matumizi mabaya ya madaraka.
Hata hivyo, mkutano huo maalumu ulimalizika kwa utata kutokana na kubainika kutotimia theluthi mbili ya wapiga kura ambayo ingeweza kumng’oa Mwita baada ya kukosekana kura moja.
Suala hilo lilichafua hali ya hewa baada ya kugundulika kuwa jina la mjumbe mmoja, ambaye hakuwepo lilikuwa limejumuishwa katika orodha ya waliohudhuria mkutano huo na kuwafanya madiwani wa Chadema kucharuka kupinga.
Baraza la madiwani wa halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam lina wajumbe 26 kati yao CCM ni 16, Chadema saba na CUF watatu.
Kwa mujibu wa kanuni za kudumu za Halmashauri ya Jiji kifungu cha 84 (1) kinaeleza ili uamuzi uweze kufanyika wa kumwondoa meya madarakani kutokana na sababu kadhaa, itapaswa kuwapo kwa theluthi mbili ya wajumbe wa halmashauri hiyo.
Theluthi mbili ya wajumbe 26 wa Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam ni 17.
Kifungu hicho kinasomeka: “Halmashauri inaweza kumuondoa meya madarakani kwa kupata azimio linaloungwa mkono na theluthi mbili ya wajumbe wa halmashauri kutokana hoja au sababu yoyote zifuatazo mojawapo ni kutumia vibaya ofisi yake.”
Hii ina maana kuwa ili Meya Mwita anayetokana na Chadema aweze kung’olewa kwa mujibu wa kifungu hicho cha 84 (1), CCM watapaswa kupata kura moja kati ya 10 za wajumbe wa upinzani.
Hata hivyo, juzi katika mkutano maalumu wa baraza hilo ulioitishwa kwa lengo la kujadili ajenda ya kumng’oa Mwita, ilishindikana kupata theluthi mbili kwani kura zilipopigwa zilikuwa 16.
Uchunguzi wa Mwananchi umegundua kutotimia theluthi mbili ya kura kulichangiwa na kukosekana kwa diwani wa Minazi Mirefu, Kassim Mshamu kutoka CUF.
Hata hivyo, jina la Mshamu lilikuwemo kwenye orodha ya wajumbe wa mkutano wa baraza la madiwani juzi kiasi cha kuzua mtafuruku baada ya wajumbe wa Chadema kudai jina la diwani huyo lilikuwa limeghushiwa.
Kimsingi Mshamu ndio kama ameushikilia umeya wa Mwita kwani kura yake sasa ni turufu ya Chadema na CCM na kutotokea kwake juzi kuliongeza utata.
Kwani inadaiwa mara ya kwanza Mshamu alikuwa miongoni mwa wajumbe waliosaini fomu kuunga mkono kuletwa mezani hoja ya kutokuwa na imani na meya.
Hata hivyo, Mshamu alipotafutwa zaidi ya mara tatu simu yake ya kiganjani iliita bila kupokelewa.
Katika mkutano wa juzi, Mkurugenzi wa Jiji, Sipora Liana alidai Mwita anakabiliwa na tuhuma mbalimbali ikiwemo kutotumia Sh5.8bilioni za Shirika la Usafiri Dar es Salaam (Uda). Fedha hizo zilitolewa na kampuni ya Simon Group kwa ununuzi wa asilimia 51 ya hisa za Uda.
Liana aliwasilisha taarifa hiyo huku akiwataka wajumbe wa CCM na Chadema waliokuwemo katika kikao hicho kupiga kura ya kutokuwa na imani na Mwita kwa mujibu wa kanuni, akisema kamati iliyomchunguza ilipendekeza jiji kufuata miongozo na taratibu katika utekelezaji wa majukumu yake na ukiukwaji wowote utachukuliwa hatua stahiki.
Mchakato wa upigaji kura ulifanyika kwa mtindo wa wajumbe wa CCM 16 kusimama kuashiria kutokuwa na imani na Mwita, wakati wale wa Chadema walikaa kuashiria kupinga hoja hiyo.
Baada ya hatua hiyo kukamilika, naibu meya wa jiji hilo, Abdallah Mtinika aliyekuwa akiongoza kikao hicho alitangaza matokeo kwa kusema “kura zilizopigwa ni 16, mjumbe mmoja ameomba udhuru na wawili hawakupiga kura, uamuzi wenu umepitishwa na kikao kimefungwa.”
Hatua hiyo ilizua mtafaruku baada ya wajumbe wa CCM kushangilia uamuzi huo huku wajumbe wa Chadema waliokuwa wanne katika kikao hicho wakisema bado wanamtambua Mwita kuwa meya wa jiji.
Hata hivyo, Mwita alijitokeza hadharani akisisitiza kuwa yeye bado ni meya wa jiji hilo kwa kuwa mkutano huo haukutimiza akidi inayotakiwa.
Katika kuonyesha yeye bado ni kiongozi wa jiji hilo, jana kwa nyakati tofauti alitinga katika ofisi za umeya zilizopo Karimjee kwa ajili ya kuendelea na majukumu yake.
Mwita alisema kuna njia mbalimbali za kumuondoa katika nafasi hiyo ikiwemo ya wajumbe wa halmashauri kugoma mara tatu kuhudhuria vikao vya baraza vitakavyoitishwa.
Wakati Mwita akieleza hayo, Mtinika aliliambia Mwananchi kuwa yeye ndiye kaimu meya wa jiji hilo baada ya juzi wajumbe wa CCM kuazimia kutokuwa na imani meya aliyekuwa madarakani.
“Hatujamtoa Mwita katika udiwani bali nafasi ya umeya, lakini ana uwezo wa kukataa rufaa kwa Waziri wa Tamisemi (Seleman Jafo). Kwa mujibu wa taratibu leo (jana) ataandikiwa barua ya kukabidhi ofisi.
“Tunatarajiwa Jumatatu (Januari 13)atakabidhi rasmi ofisi pamoja makabrasha mbalimbali. Leo nasafiri kuelekea Zanzibar kwenye sherehe za Mapinduzi, nikirudi kila kitu kitakuwa sawa,” alisema Mtinika.
Ufafanuzi wa Mkurugenzi wa Jiji
Mkurugenzi wa Jiji la Dar es Salaam, Liana amedai wajumbe 16 ambao walipiga kura ya kutokuwa na imani na meya walifikisha theluthi mbili.
Alidai kanuni ya kumuondoa meya ilikuwa inaelekeza theluthi mbili ya wajumbe waliodhudhuria mkutano huo.
Liana alishikilia kuwa uamuzi uliofanywa katika mkutano wa juzi ulikuwa ni halali.
Alipoulizwa kwa nini Mwita bado anaendelea kutumia ofisi ya jiji alisema, “alikuwa anatumia kwa sababu tulikuwa hatujampa barua, tayari tumempa. Tumuone basi kama atatumia, tutaona kama ataendelea sasa.”
Wakati huohuo, Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu ilitupilia mbali ombi la Mwita la kuitaka itoe zuio la muda ili asiondolewa kwenye nafasi yake hadi kesi ya msingi itakaposikilizwa na kutolewa uamuzi.
Uamuzi huo mdogo uliotolewa na Hakimu Mkazi Mkuu Janeth Mtega aliyesema haikuona uthibitisho mahakamani hapo kuhusu uwepo wa kikao cha kumuondoa madarakani Mwita wala hasara atakayoipata endapo ataondolewa.
Hakimu Mtega licha ya kutoa uamuzi huo pia alipanga kusikiliza kesi ya msingi ya Mwita ya kupinga mchakato wa kumng’oa, umeya Jumatatu ijayo
Tags