Bilionea wa Japan afuta mpango wa kumtafuta 'mpenzi wa maisha' kwenda naye mwezini



Bilionea wa Japan aliyekuwa akitafuta mwanamke "mpenzi wa maisha" wa kwenda naye mwezini amefutilia mbali mpango huo

Tajiri huyo ambaye pia ni mwanamitindo maarufu alikuwa ametoa mualiko kwa wanawake walio na umri wa chini ya miaka 20 ambao hawajaolewa wawasilishe maombi yao "kwa safari hiyo ya kipekee ya kimahaba".

Karibu wanawake 28,000 walitoa maombi, lakini siku ya Alhamisi alisema kuwa amepatwa na "hisia mseto" kuhusiana na suala hilo ndiposa akaamua kufutilia mbali wazo hilo.

Bado ana mpango wa kuendelea mbele na ziara yake mwezini mwaka 2023- bila mpenzi.

Mapema mwezi Januari, bilionea huyo wa miaka 44 alitoa tangazo mtandaoni kumtafuta mpenzi wa kike atakayeandamana naye mwezini.

Tovuti yake ilikuwa imeweka masharti pamoja na maelezo kuhusu jinsi ya kuwasilisha maombi katika mchakato huo uliochukua miezi mitatu.

Katika ombi la mtandaoni, Bw. Maezawa anasema kuwa anataka kufurahia safari hiyo na mwanamke wa kipekee.

Masharti ya kushiriki lazima uwe bila mpenzi, uwe na miaka zaidi ya 20, uwe na mtazamo mzuri wa maisha na ufurahie kuzuru anga za mbali.

Muda wa mwisho wa kuwasilisha maombi ni Januari 17 ambapo uamuzi wa mwisho kuhusu mpenzi wa Bw. Maezawa ulikuwa utatolewe mwisho wa mwezi Machi.

Lakini siku ya Alhamisi ,aliweka tangazo katika Twitter akisema kuwa hana haja tena ya kutafuta mpenzi wa kwenda nae mwezini.

"Nimepatwa na hisia mchanganyiko kuhusu kushiriki kwangu," alisema katika moja ya ujumbe wake kwenye twitter.

''Kuona kwamba wanawake 27,722 wenye malengo walitumia wakati wao mwingi kuwasilisha ombi kunanifanya kujuta na kuambia kila mtu kuhusu uamuzi wangu wa kibinafsi''

Bilionea huyo ambaye amejizolea sifa kwa kuwa mpiga ngoma katika bendi ya punk, anajulikana kwa kujihusisha na visa ambavyo huzua gumzo na kuwaacha watu midomo wazi.

Hii sio mara ya kwanza Bw Maezawa, kutoa tangazo kama hili ambalo limezua gumzo mitandaoni.

Aliwahi kutoa ahadi ya kupeana Yen milioni 100m sawa na ($925,000; £725,000) kwa watu 100 watakaosambaza ujumbe wake wa twitter.

"Unachotakiwa kufanya ili kushiriki ni kunifuatilia kwa kutweet tena (Retweet)," alisema.

Posti hiyo imesalia kuwa maarufu kwa ujumbe uliopata retweet nyingi zaid

Inaripotiwa kuwa aliwatangaza washindi mwezi Januari mwaka uliopita wa 2019.

Mwanzilishi huyo wa biashara ya kuuza nguo mtandaoni nchini Japan Zozo Inc, Bw. Maezawa alijizolea utajiri mkubwa katika ulimwengu wa uanamitindo.

Anaamniwa kuwa na utajiri wa karibu $3bn, sehemu kubwa ya pesa hizo anatumia katika sanaa.

Mwaka 2018, Bw Maezawa alitajwa kuwa abiria wa kwanza kwenda mwezini kwa kutumia roketi maalumu inayofahamika kama ''Starship''.

Safari hiyo iliyopangiwa kufanyika mwaka 2023, itakuwa ya kwanza kwa binadamu kwenda mwezini tangu mwaka 1972.

Kiasi cha fedha ambazo Bw. Maezawa amekubali kulipa kama nauli kwenda mwezini hakijawekwa wazi, lakini inadaiwa kuwa ''pesa nyingi sana''.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad