Baraza la wawakilishi la bunge la Marekani litapiga kura leo ya kudhibiti uwezo wa Rais Donald Trump kuchukua hatua za kijeshi dhidi ya Iran wakati shutuma za Wademocrat dhidi ya mashambulizi ya Marekani yaliyomuua jenerali wa ngazi ya juu ya Iran zikiendelea.
Spika wa Baraza hilo, Nancy Pelosi , alitangaza kura hiyo katika taarifa ambayo inasema shambulio la wiki iliyopita la ndege isiyo na rubani ambalo limemuuwa Jenerali Qassem Soleimani ni la uchokozi na limevuka mipaka.
Azimio la chama cha Democratic la madaraka ya vita linaonekana litapitishwa dhidi ya upinzani mkali wa chama cha Republican. Pendekezo kama hilo la Seneta Tim Kaine wa chama cha Democratic, linakabiliwa na mapambano makali katika baraza la Seneti kutoka kwa maseneta wa chama cha Republican.
Kutokana na mzozo wa kiutendaji baina ya vyama hivyo viwili, haifahamiki iwapo kura ya leo itakuwa hatua kuelekea kumzuwia Trump kuhusu Iran ama itakuwa ni ishara tu ya upinzani wa Wademocrat.