Baraza la seneti nchini Marekani limepiga kura kwa misingi ya chama na kuidhinisha sheria zitakazotumika katika kesi ya kumuondoa madarakani Rais Donald Trump.
Baraza hilo lililo na idadi kubwa ya maseneta wa chama cha Republican limezikataa juhudi za Wademocrat za kupata ushahidi na kuhakikisha kwamba mashahidi wanasikilizwa.
Wakili mkuu wa Trump katika kesi hiyo amesema kesi ya Wademocrat ni juhudi zisizo na msingi kutaka kupindua ushindi wa Trump katika uchaguzi wa mwaka 2016 ingawa mbunge mmoja wa chama cha Democratic amesema kuna ushahidi wa kutosha kuonyesha makosa ya Trump.
Baraza la wawakilishi la bunge la Marekani lilipiga kura ya kumuondoa madarakani Trump mwezi uliopita kutokana na madai ya matumizi mabaya ya madaraka na kuzuwia mamlaka ya bunge la Congress kwa kuishinikiza Ukraine kumchunguza hasimu wake wa kisiasa ambaye ni makamu wa rais wa zamani Joe Biden wa chama cha Democratic.
Trump anashikilia hakufanya makosa yoyote.