Bunge lamtaka Mwanasheria mkuu wa Serikali kulitazama suala Mbunge Zitto Kabwe kutumia nembo ya Bunge




Na. Immaculate Makilika – MAELEZO
Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Job Ndugai amemuomba Mwanasheria Mkuu wa Serikali Dkt. Adelardus Kilangi kulitazama suala Mbunge  Zitto Kabwe kutumia nembo ya Bunge katika barua inayotaka Benki ya Dunia  kusitisha mkopo wa nafuu wa elimu  dola milioni 500  wenye lengo la kuboresha elimu nchini.

Akizungumza leo Bungeni jijini Dodoma katika kipindi cha maswali na majibu, Spika wa Bunge, Job Ndugai alisema kuwa hatua ya Mbunge wa Kigoma Mjini Zitto Kabwe, kuandika barua Benki ya Dunia kwa kutumia nembo ya Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuitaka benki hiyo isitishe mkopo huo kwa muda ni kutumia vibaya nembo ya Bunge, na  kuwa huo si msimamo wa Bunge.

“Katika jambo hili kuna dalili za ujinai, kwa hiyo tunakuomba Mwanasheria Mkuu wa Serikali uchunguze na mkiona kuna ujinai  muweze kuchukua hatua, sisi kama wabunge hatujafurahishwa na jambo hili” alisema Spika Ndugai

Spika Ndugai alifafanua kuwa ikiwa Mbunge ana tofauti za kisera ni vyema kurekebisha kwa muktadha huo kuliko kusababisha nchi nzima kukosa fursa kwa sababu tu ya kutokubaliana  na jambo fulani.

Kwa upande wake, Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Dkt. Adelardus Kilangi alisema kuwa ofisi yake imepokea maelekezo hayo na itayafanyia kazi kwa mujibu wa sheria zilizopo.

Januari 28 mwaka huu, katika hafla ya kuapisha viongozi mbalimbali iliyofanyika Ikuku jijini Dares salaam, Rais Dkt. John Pombe Magufuli, alisema kuwa Makamu wa Rais wa Benki ya Dunia alikuja nchini Tanzania mwaka 2019 kwa ajili ya mazungumzo na hivyo wanapotoa hizo fedha wanajua msimamo wa nchi na kuwataka viongozi kutojibishana na baadhi ya watu wanaopotosha kuhusu suala hilo.

Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad