DC Temeke Kutumia Mahakama Inayotembea Kutokomeza Uchangudoa


Mahakama
Mkuu wa Wilaya ya Temeke, Bw.Felix Lyaniva amesema kwamba atahakikisha anatumia huduma ya gari maalum la Mahakama Inayotembea mara kwa mara ili kutokomeza vitendo vya biashara ya uchangudoa, uhalifu, unywaji wa pombe za saa za kazi, uhalifu, uzururaji na uchafuzi wa mazingira katika eneo lake.

Kauli hiyo imetolewa leo Januari 24, mwaka huu wakati Mahakama hiyo, ilipokuwa ikiendesha mashauri yaliyoletwa mahakamani hapo kwa ngazi ya Mahakama ya Hakimu Mkazi Sokoine Drive maarufu kama ‘Mahakama ya Jiji’ baada ya Manispaa ya Temeke, kufanya operesheni maalum na kuwakamata watuhumiwa hao wa makosa hayo.

Huduma hiyo iliyokuwa ikitolewa katika viwanja vya Zakhem vilivyoko Mbagala jijini Dar es Salaam.

‘Mahakama Inayotembea ni suluhisho la kutokomeza vitendo vya biashara ya uchangudoa, uhalifu, unywaji wa pombe saa za kazi na uhalifu. Tunataka watu wafanye kazi halali na kufuata sheria za nchi,’ alisema Lyaniva huku akiongeza kwamba hataki kuona vitendo hivyo kwenye eneo lake.

Alisema watuhumiwa hao, walikamatwa na ushahidi ukiwepo. Lyaniva aliongeza kwamba anaiomba Mahakama ya Tanzania, kutoa huduma hiyo mara kwa mara kwenye wilaya hiyo, ikiwezekana kwa kila Ijumaa. Akizungumza kuhusu watuhumiwa waliofikishwa mahakamani hapo, Mratibu wa Mahakama hiyo, Mhe Moses Ndelwa, ambaye pia ni Hakimu Mkazi alisema wako takribani 50.

Hivyo mashauri hayo yanasikilizwa, baada ya kupokea maelezo kutoka kwa waendesha mashitaka na wapelelezi. Ndelwa alifafanua kwamba watuhumiwa hao wametonzwa faini ya Sh. 20,000 hadi 50,000 kulingana na makosa waliyotenda.

Naye Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Wilaya ya Temeke, Mhe. Suzan Kihawa alisema watuhumiwa hao , wanakiri makosa ndio maana makosa yao hayahitaji uchunguzi hali sababisha kusikilizwa kwa haraka. Mashauri hayo yalisikilizwa na Hakimu Mkazi Mkuu wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Sokoine Drive.

Wakati huohuo, baadhi ya wakazi wa Mbagala, wakizungumza kwa nyakati tofauti, ambao ni Adamu Juma alisema tukio hilo limemfundisha kwamba unaweza kukamatwa na kuhukumiwa hapo kwa hapo.

Wengine ni Hamisi Ally umri wa miaka (22), Said Hemed (20), Eva Michael(40) na Abuu Ramdhani walisema wanaishukuru Serikali kwa kuleta huduma hiyo, ambayo inakwenda vizuri na kuwezesha mashauri kusikilizwa kwa wakati na kupunguza mlundikano wa mahabusu au kesi kuchukua muda mrefu.
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad