Fundi Simu Wasiosajiliwa Mwisho Julai, TCRA yatangaza Kibano


Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) Kanda ya Kaskazini imetangaza kibano kwa mafundi wa vifaa vya kielektroniki zikiwamo simu za mkononi wasiosajiliwa na kwamba hawataruhusiwa kufanya kazi hiyo.

TCRA imesema kibano hicho kitaanza rasmi Julai, mwaka huu, na kwamba hakuna fundi ambaye atafanya kazi kama hajasomea wala kusajiliwa hivyo imewataka mafundi hao kujiunga kwenye kikundi ili kupatiwa elimu.

Mwanasheria wa TCRA, Kant Mosha, amesema hayo juzi katika mkutano wa mafundi wa vifaa vya kielektroniki uliofanyika kwenye ukumbi wa ofisi ya mkuu wa mkoa wa Arushamambapo aliwataka mafundi kuwa na usajili wa kikundi.

Amesema mafundi simu ni kada ambayo ilikuwa imesahauliwa lakini kuanzia sasa, serikali imeamua kuwatambua, hivyo kuungana ni sehemu ya kufanikiwa kwa malengo yao.

Mwenyekiti wa Chama cha Mafundi Simu Kanda ya Ziwa, Maguwa Manyanda, aliwataka kutambua kwamba mafundi simu ni wa thamani kwa kuwa jamii inawategemea na wanachangia mapato ya serikali.\

Alisema mafunzo hayo yataondoa changamoto na kuwafanya kuwa huru katika shughuli zao za kila siku, hivyo umoja ni nguzo ya kuwafikisha kushirikiana na serikali katika masuala mbalimbali vikiwamo vyombo vya dola.

Manyanda ameongezea kuwa ili kila moja atende kazi zake ni muhimu akajiunga na umoja huo ili kuondoa changamoto zao ambazo zimekuwa zikiwafanya kukumbana na misukosuko kutoka polisi.

Naye Mwenyekiti wa Umoja wa Mafundi Simu Kanda ya Kaskazini, Nasri Mtengeti, amesema wamefurahi kupata elimu hiyo ya umoja ambayo itawasaidia kuondokana na changamoto mbalimbali.

Awali, akitoa mafunzo kwenye mkutano huo, Mratibu wa Vikundi hivyo kutoka TCRA, Mhandisi Kadaya Buluhye, aliwataka mafundi hao kufanya kazi kwenye umoja kwa lengo la kupata elimu na usajili.

Alisema Jeshi la Polisi linafanya kazi ya kulinda usalama na mali za raia, lakini umoja wao utasaidia kufanya kazi kwa karibu na jeshi hilo na kuondoa changamoto ambazo wamekuwa wakikumbana nazo kama mafundi.
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad