Iran imetangaza leo kwamba watu kadhaa wamekamatwa kuhusiana na kombora lililorushwa kimakosa na kuiangusha ndege ya Ukraine karibu na uwanja wa ndege wa Tehran, na kuwauwa watu wote 176 waliokuwa ndani ya ndege hiyo.
Tangazo hilo limekuja muda mfupi baada ya Rais Hassan Rouhani kutaka iundwe mahakama maalum kushughulikia mkasa huo. Msemaji wa idara ya mahakama, Gholamhossein Esmaili, aliyetoa tangazo hilo, hakubainisha idadi ya watu waliotiwa mbaroni.
Huku hayo yakiarifiwa, wanadiplomasia wa nchi za Magharibi, wamesema mataifa matatu ya Ulaya yaliosaini mkataba wa kimataifa kuhusu mpango wa nyuklia wa Iran, Uingereza, Ufaransa na Ujerumani, hii leo yatakitumia kifungu cha kujadili mizozo katika mkataba huo uliosainiwa mwaka 2015.
Tayari Marekani imejiondoa katika makubaliano hayo, na Iran imesema itaacha kuheshimu ukomo wa kurutubisha madini ya urani uliowekwa katika makubaliano hayo.