WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Rais-TAMISEMI, Mhe Selemani Jafo amemuagiza Mkurugenzi wa Jiji la Dodoma, Godwin Kunambi kumuongeza mshahara Dereva wa Kijiko cha kusomba takataka na kuzikandamiza kwenye dampo la Chidaya wilaya Dodoma, Esther Nyange.
Uamuzi huo umefikiwa baada ya Waziri Jafo kuvutiwa na uthubutu wa dereva huyo mwanamke wa kufanya kazi ngumu ambayo hata baadhi ya wanaume wameshindwa kuifanya.
Ameyasema hayo katika ziara ya kukagua dampo hilo la kisasa ambapo amesema hajaridhishwa na maendeleo yake baada ya kukuta mrundikano wa taka nyingi ambazo hazijafanyiwa kazi.
" Mkurugenzi kiasi cha Sh Laki Mbili mnazomlipa huyu Dada hakilingani na kazi kubwa anayofanya, sitaki nikupangie kiasi cha kumlipa lakini hakikisha unamuongezea na kuboresha maslahi ya mkataba wake," Amesema Mhe Jafo.
Akizungumzia hali ya dampo Waziri Jafo amesema ni Jambo la aibu kuona licha ya dampo hilo kujengwa kwa gharama kubwa lakini watumishi wake wameshindwa kulisimamia vizuri kiasi cha kukuta takataka zikiwa katika hali ambayo haieleweki.
" Mkurugenzi mmesema kuna vifaa vilikua vimeharibika na sasa mmeshavitengeneza ninawapa wiki mbili hali ya dampo hili iwe ya kupendeza, kueleweka na ifanane na hadhi ya makao makuu ya Nchi.
Hiki kijiko ambacho anaendesha huyu Dada mmesema kimekaa miezi miwili bila kufanya kazi huu nao ni uzembe na ninawapa pia wiki mbili kuhakikisha kijiko hiki kinafanya kazi ili huyu Dada aendelee na kazi," Amesema Mhe Jafo.