Na Faustine Gimu
Jeshi la Polisi Mkoa wa Dodoma limemkamata Boniface Mushi ambaye ni mlinzi wa Ofisi za TANESCO baaada ya kuvunja ofisi za hizo eneo la area D jijini Dodoma na kuiba kompyuta mpakato[Laptop].
Akizungumza na waandishi wa habari leo Jan,27,2020 jijini
Dodoma,Kamanda wa Polisi mkoani hapa Girres Muroto amesema msako mkubwa ulifanyika katika eneo hilo ambapo mlinzi wa kampuni binafsi ya ulinzi QSS Deus Mushi alikamatwa katika eneo la wilaya ya Kwimba Mkoani Mwanza baada ya kuiba laptop hiyo kutoka Dodoma katika
ofisi za TANESCO, za mradi wa miundombinu ya umeme shirikishi ya nchi tatu ambazo ni Tanzania ,Kenya na Zambia.
Katika tukio jingine kamanda Muroto amesema katika Mtaa wa Kizota jijini Dodoma alikamatwa Joshua Elisha [38] mlinzi wa Kampuni ya ulinzi ya KK Security mkazi wa Kizota Mbuyuni akiwa na Compresssor ya friji kubwa ambayo ni mali ya wizi aliyoiba baada ya kuvunja store ya lindo .
Aidha,Kamanda Muroto amesema jeshi hilo limeokota Jumla ya pikipiki nne katika maeneo tofauti zikiwa zimetelekezwa na wahalifu wakati wa doria ambapo wenye pikipiki walikimbia baada ya kukurupushwa wakiwa kwenye harakati za kufanya uhalifu na pikipiki hizo ni MC.813 CDH Fekon nyekundu MC .128 CCQ BOXER nyekundu MC 857 CCU TVS nyekundu naT. 967 CKK BOXER nyeusi ambapo imebainika kuwa ni Namba bandia.
Pia,Jeshi hilo limefanikiwa kukamata nyara za serikali huku likiwaasa wananchi kuchukua tahadhari dhidi ya wahalifu mbalimbali nchini wakiwemo waendesha bodaboda nyakati za usiku.