RAIS John Magufuli ameagiza makontena ya makinikia yaliyokamatwa yauzwe kwa wateja na faida iende kwenye kampuni mpya ya Twiga, inayomilikiwa na serikali na kampuni ya madini ya Barrick.
Ametoa maagizo hayo wakati akihutubia baada ya kushuhudia utiaji saini makubaliano kati ya serikali ya Tanzania na Kampuni ya Madini ya Barrick leo Ijumaa, Januari 24, 2020, asubuhi Ikulu, Dar es Salaam, na kuongeza kuwa utiaji saini huo ni ushindi mkubwa.
“Hata yale makontena tuliyoyashika sasa fanya utaratibu mzuri yarudi katika Kampuni ya Twiga mtafute wateja. Najua yameshauzwa na mteja yupo na ameshalipa kiasi fulani. Pamoja na stori kuwa zilikuwa zinapelekwa kuyeyushwa. Si kweli, yalikuwa yanauzwa.
“Siwezi kuwa rais na mali inasombwa mnaambiwa ni mchanga, mnakubali na polisi wanasindikiza. Sasa kama ni mchanga kwanini unalindwa? Na kuzunguka eneo la mgodi watu wana njaa, hawana elimu, madawa wala maji. Haikuwa sawa,” alisema.
Aidha, amewaeleza wawekezaji kuwa Tanzania ni eneo bora zaidi kwa uwekezaji hasa ikizingatiwa kuwa nchi tajiri yenye kila aina ya rasilimali.
“Sisi hatupo hapa kugombana na mwekezaji yeyote, tupo hapa kushirikiana nao katika hali ya kila upande kushinda. Barrick muwe na uhakika hapa ni mahali pa kukaa, mtakaa hapa leo, kesho na daima kwa sababu tunaona nyie ni wadau wazuri.
“Nawashukuru Barrick kwa busara, mngeweza kusema tunatumia ‘force’ ila sina hakika kama mngeichimba hiyo dhahabu. Sina hakika, lakini mmetumia busara, hiyo ni nzuri sana na serikali yangu itoa ushirikiano mzuri sana ili mchimbe mpate faida na sisi tufaidike. Fikiria kutoka ‘share’ ya sifuri hadi ya 16%, lakini pia faida itakayopatikana ni 50 kwa 50 ni ushindi mkubwa kwa pande zote mbili.
“Mheshimiwa Kabudi mengine hakuyaeleza alivyokuwa anapata misukosuko na kuteseka, nilikuwa nampigia wakati mwingine usiku saa saba…
“Ninajua tumetoka mbali, wakati yale madini yalivyokuwa yakisombwa kwenye miaka mingi, na Watanzania tukaambiwa tuamini kwamba ni mchanga na kweli Watanzania wengi wakaamini ni mchanga, lakini swali la kujiuliza tu kama ni mchanga kwa nini usafirishwe?” amesema.
#LIVE: HOTUBA YA RAIS MAGUFULI MBELE YA KAMPUNI YA BARRICK