Kamera ya Kwenye Kiyoyozi yatumika Katika Uchunguzi wa Kesi ya Mwanaharakati
0
January 28, 2020
Mwaka mmoja baada ya mwanaharakati wa upinzani Anastasia Shevchenko kuwekwa katika kifjungo cha nyumbani, amegundua kuwa kamera ya uchunguzi iliwekwa katika chumba chake cha kulala na kuchukua picha za kila kitu kwa miezi kadhaa.
Picha zilizochukuliwa ni pamoja na zile alizokua amevaa nguo ya ndani, zilizokusanywa walipokua wakitafuta ushahidi wa kumuweka hatiani kwa uanaharakati wa kisiasa.
Mazungumzo yake ambayo pia yalinaswa, yameelezea kukasirishwa sana na kile walichokiita "hatua ya kuwadhalilisha sana" iliyotekelezwa na mamlaka.
Bi.Shevchenko, mwenye umri wa miaka 40, amepigwa marufuku kuwasiliana na watu wengine kutoka katika nyumba ya gorofa lililopo katika mji wa kusini wa Rostov on Don.
Mtoto wake wa kike, Vlada, anasema mama yake aligundua kutoka kwa wachunguzi kwamba walikua wameweka mitambo kwenye makazi ya familia, walipokua wakimpelekea kurasa za nyaraka za maelezo ya maandishi.
"Mwezi uliopita , wachunguzi walionyesha picha zake na akagundua kuwa wamekua wakichukua filamu yake pia ," Vlada aliiandikia BBC.
" Katika picha hizo tuligundua kuwa walikua wameweka kamera mkabala na kitanda cha mama yangu, eneo la kiyoyozi ."
Vlada, ambaye anatunza blogi ya maisha ya familia yake, aliandika kwenye ukurasa wa Facebook kwamba utambuzi wa kuchukuliwa kwa filamu ya maisha yake na familia yake ilikua ''aibu ,ndio kwa wanaume waliovaa mapete ya vyeo", akimaanisha maafisa wa huduma za usalama.
Tamara Gryaznova alishitushwa sana na kuingiliwa kwa maisha ya binti yake
Lakini mama yake na Bi Shevchenko, anayeishi na Anastasia na watoto wake wawili.
Alikiri kuwa wamekuwa wakisumbuliwa sana na ugunduzi wa filamu za uchunguzi wa binti yake, "Kulikua na picha zake akiwa amevalia sindiria tu , watoto walikuwa katika picha hizo pia. Kusema kweli hazikuwa nzuri," Tamara Gryaznova aliiambia BBC.
Anastasia Shevchenko yuko katika kifungo cha ndani na amezuiwa kuwasiliana na dunia
"Kulikua na video na vinasa sauti vya kurekodi mazungumzo yetu. Sasa wachunguzi wanamfanya apitie rekodi zote na picha ili kuthibitisha kama ni halisi. Hatukutarajia kwamba watatudhalilisha kiasi hiki ."
Wakili wa familia, Sergei Badamshin, amethibitisha kwamba vifaa vya uchunguzi viliwekwa kwa siri katika nyumba ya familia katika majira ya kipupwe mwaka 2018, na kwamba viliidhinishwa na mahakama ya eneo hilo.
Baadae alishtakiwa kwa kuwa mjumbe wa " kundi lisilolotakiwa ", chini ya sheria ya mwaka 2015, kwa uhusiano na kikundi kilichoanzishwa na Mikhail Khodorkovsky, mtawala wa zamani tajiri mkubwa ambaye sasa ni mkosoaji mkuu wa utawala wa Kremlin.
Bwana Badamshin alikejeli matokeo ya operesheni ya upelelezi wa miezi mitano akiusema "usio na maana", ikizingatiwa kuwa ushahidi wa shuguli za mteja wake zinaangaliwa kama "tishio… kwa usalama wa taifa na katiba" kwa kushiriki mkutano wa haki za binadamu na maandamano ya mtaani ambayo hayakuidhinishwa.
Lakini ni uingiliaji wa maisha ya ndani ya binafsi ya Bi Shevchenko ambayo yameitatiza familia yake.
" Wangeweza kuweka kamera kwenye meza," Tamara Gryaznova alisema "Lakini wameiweka juu ya kitanda cha Nastya."
Katika kesi hii , uchunguzi ulikua ni sehemu ya upelezi wa uhalifu- unaoadhibiwa kwa adhabu ya kifungo cha miaka sita gerezani.
Lakini imekumbusha baadhi ya nyakati za nyuma ambazo hazikuwa nzuri katika siasa za Urusi.
"Kutambua kuwa kulikua na kamera katika chumba chako cha kulala kwa miezi ni zaidi ya inatia kiwewe cha hali ya juu, " Natalia Pelevina wa chama cha upinzani cha Parnas alisema.
Natalia Pelevina anaamini wanaharakati wa upinzani wanakabiliwa na shinikizo la kisaikolojia
Mnamo mwaka 2016, picha zake akiwa kitandani zilizochukuliwa kwa siri akiwa na waziri mkuu wa zamani Mikhail Kasyanov zilitangazwa hewani katika televisheni ya taifa kama sehemu ya kampeni ya kumharibia sifa.
"Unahisi kama umeharibiwa na kuibiwa," aliimbia BBC , na kuongeza kuwa uamuzi wa kesi ya Bi Shevchenko pia ulikua na malengo mengine zaidi ya kukusanya ushahidi.
"Ni shinikizo la kisaikolojia wanalojaribu kutumia, pamoja na kupandikiza hofu kwa wajumbe wengine wa upinzani ," anaamini.
Familia ya Shevchenko ilihamia kwenye nyumba nyingine lakini Tamara Gryaznova anasema wameachwa na hisia za wasiwasi.
Tags