Bilionea wa Japan Yusaku Maezawa anamtafuta mwanamke atakayekuwa "mpenzi wa maisha" ili aandamane naye kutalii anga za mbali hadi mwezini.
Mwanamitindo huyo wa miaka 44, anajiandaa kuwa abiri wa kwanza kwenda mwezini kwa kutumia roketi maalumu inayofahamika kama ''Starship''.
Safari hiyo iliyopangiwa kufanyika mwaka 2023, itakuwa ya kwanza kwa binadamu kwenda mwezini tangu mwaka 1972.
Katika ombi la mtandaoni, Bw. Maezawa anasema kuwa anataka kufurahia safari hiyo na mwanamke wa kipekee.
Mfanyibiashara huyo ambaye hivi karibuni aliachana na mpenzi wake muigizaji Ayame Goriki mwenye umri wa miaka 27, ametoa wito kwa wanawake kuwasilisha maombi yao kuhusu"safari hiyo ya kipekee" katika tuvuti yake.
"Japo hisia ya upweke imeanza kunizonga, nafikiria kitu kimoja: kuendelea kumpenda mpenzi wangu," Bwana Maezawa aliandika katika tuvuti yake.
"Nataka kumpata 'mpenzi wa maisha'," Bwana Maezawa. "nikiwa na mpenzi wangu mtarajiwa wa maisha, nataka kuutangazia ulimwengu penzi letu nikiwa mwezini."
Tovuti hiyo imeweka masharti pamoja na maelezo kuhusu jinsi ya kuwasilisha maombi katika mchakato huo utakaochukua miezi mitatu.
Masharti ya kushiriki lazima uwe bila mpenzi, uwe na miaka zaidi ya 20, uwe na mtazamo mzuri wa maisha na ufurahie kuzuru anga za mbali.
Muda wa mwisho wa kuwasilisha maombi ni Januari 17 ambapo uamuzi wa mwisho kuhusu mpenzi wa Bw. Maezawa utatolewa mwisho wa mwezi Machi.
Bilionea huyo ambaye amejizolea sifa kwa kuwa mpiga ngoma katika bendi ya punk, anajulikana kwa kujihusisha na visa ambavyo huzua gumzo na kuwaacha watu midomo wazi.
Mapema mwezi huu, Bw. Maezawa aliahidi kupeana yen milioni 100m sawa na ($925,000; £725,000) kwa watu 100 watakao share ujumbe wake wa twitter .
"Unachotakiwa kufanya ili kushiriki ni kunifuatilia kwa kutweet tena (Retweet)," alisema.
Mwanzilishi wa biashara tya kuuza nguo mtandaoni nchini Japan Zozo Inc, Bw. Maezawa alijizolea utajiri mkubwa katika ulimwengu wa uanamitindo.
Anaamniwa kuwa na utajiri wa karibu $3bn, sehemu kubwa ya pesa hizo anatumia katika sanaa.