Rais wa Kenya Uhuru Kenyatta amefanya mabadiliko katika Baraza la Mawaziri. Katika hotuba yake ya kwanza katika mwaka wa 2020 aliyoitoa kwenye Ikulu ya Rais Mombasa amemteua Monica Juma kama waziri wa ulinzi huku Raychelle Omamo akiwa waziri wa mambo ya nje.
Ukur Yatani ameteuliwa kama waziri wa fedha, Mutahi Kagwe waziri wa Afya huku Betty Maina akichukua wizara ya viwanda na Sicily Kariuki akiwa waziri wa maji.
Esther Koimett waziri wa habari na mawasiliano. Simon Chelugui ni waziri wa Leba. Peter Munya ndio Waziri wa kilimo huku Mwangi Kiunjuri akipigwa kalamu na wengineo.
Wakati wa hotuba yake Rais amesema kwamba wanaweka mipango ya kukwamua uchumi na kuweka wazi kuwa asilimia 70 ya madeni yamelipwa.
Pia ameweka kipau mbele katika biashara na kusema kuwa juhudi zinafanywa kusaidia biashara ndogo ndogo. Pia ametaka nchi kutoa umuhimu kwa uchumi badala ya siasa.
Aidha, rais amesema kwamba anaamini hakuka utawala ambao umekabiliana na ufisadi kama alivyofanyika kwenye utawala wake. ''Kuanzia mawaziri mpaka magavana, maafisa wakuserikali, maafisa wa ununuzi, nimekuwa mstari wa mbele. Rais Uhuru ameonyesha imani kuwa ufisadi umeogopesha wezi wa mali ya umma na kuacha mpira kwa mfumo wa mahakama akiitaka iwajibike kuhakikisha kuwa nchi inashinda vita dhidi ya ufisadi.
Miongoni mwa aliyoyazungumzia ni utoaji wa fedha za ujenzi wa viwanda viwili vya maziwa.